Waziri Mkuu akutana na kampuni za madini kutoka Korea Kusini

DAR ES SALAAM-Waziri MKUU Kassim amekutana na ujumbe kutoka Korea Kusini uliojumuisha viongozi wa makampuni makubwa ya madini yanayohusika na mnyororo wa thamani wa uzalishaji betri za magari ya Posco Holdings, Posco International,SK, Korea Zinc na LX International.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Korea Kusini ulioambatana na kampuni kubwa za madini, nje ya Ukumbi wa BoT jijini Dar es salaam, Septemba 2, 2023.

Mheshimiwa Majaliwa amewahakikishia wawekezaji hao kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kwa uwekezaji wao na itawawezesha kuwekeza mitaji yao.

“Sisi tuna madini na ninyi ndugu zetu Wakorea mna mitaji, twende tuunganishe nguvu kwa manufaa ya nchi zote.”alisema.


Ameyasema hayo Jumamosi, Septemba 2, 2023 alipokutana na ujumbe wa Korea Kusini na kujadili kuhusu uhushirikiano katika uendelezaji wa madini ya kimkakati nchini Tanzania.

“Ninapenda kuwahakikishia kuwa nchi yetu ni salama na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kila linalowezekana kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini.”

Waziri Mkuu amesema Serikali imeimarisha mazingira ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya usafirishaji kama barabara, ndege na nishati ya kutosha kwa ajili ya uendeshaji wa viwanda. “Lengo ni kuhakikisha kila muwekezaji anayekuja anapata faida kutokana na uwekezaji wake.”

Kwa upande wake, Mjumbe Maalumu wa Rais wa Korea ambaye ndiye kiongozi wa ujumbe huo kutoka Korea Kusini, Bw. Yoon Sang Jick ameishukuru Serikali ya Tanzania na kwamba wataendelea kushirikiana nayo kuhakikisha malengo ya uwekezaji yanafanikiwa.

Naye, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameishukuru Korea Kusini kwa kuichagua Tanzania nna kufanya mazungumzo kuhusu uwekezaji katika sekta ya madini. Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini humo waje wawekeze Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news