Yanga SC yaishusha kileleni Mashujaa FC

DAR ES SALAAM-Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam imeishusha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Mashujaa FC ya mkoani Kigoma.
Ni baada ya bao la Mudathir Yahya Abbas dakika 88 dhidi ya Namungo FC kutoka mkoani Lindi kubadili mwelekeo wa mtanange ambao ulionekana wa moto.

Mtanage huo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara umepigwa leo Septemba 20, 2023 katika Dimba la Chamazi Complex lililopo Kata ya Chamanzi, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Abbas alifunga bao hilo kwa kupenyeza mguu katikati ya mlinzi Derrick Mukombozi na kipa wa Namungo FC, Deogratius Munishi (Dida) kuunganishia nyavuni krosi ya winga Jesus Moloko.

Mfungaji na mtoa pasi ya bao waliinuliwa kwa pamoja kutokea benchi dakika ya 67 kuchukua nafasi ya mshambuliaji Clement Mzize na kiungo Pacome Zouazoua.
Namungo FC wameingia dimbani huku wakiwa na majonzi baada ya kupoteza mashabiki wake wanne waliofariki katika ajali na wengine kadhaa kujeruhiwa ambapo walikuwa wanasafiri kuja kushuhudia mtanange huo.

Awali taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Namungo FC ilifafanua kuwa, ”Uongozi wa Klabu ya Namungo FC umepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya mashabiki wetu waliokuwa wakisafiri kutoka Ruangwa kuelekea Dar es Salaam kuishangilia timu yao kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Yanga SC mchezo utakaofanyika leo tarehe 20 Septemba 2023.”

”Ajali hiyo imetokea eneo la Miteja karibu na Somanga na kupelekea vifo vya mashabiki wetu wanne (4) na majeruhi kumi na sita (16). Kwa sasa majeruhi wote wamepelekwa katika kituo cha afya Tingi Wilaya ya Kilwa, Lindi.”

”Klabu ya Namungo FC tunatoa pole kwa wanaruangwa, mashabiki, Familia na Kwa wote waliopata ajali hiyo na majeruhi tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu wpone haraka.Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahala pema Amina."

Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetoa salamu za pole kufuatia vifo vya mashabiki wanne wa Namungo FC na wengine 16 kujeruhiwa kwenye ajali hiyo.
Hata hivyo, ushindi huo unaifanya Yanga SC ifikishe alama tisa na kurejea kileleni ikiizidi alama mbili Mashujaa FC baada ya wote kucheza mechi tatu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news