LATRA yabaini ujeuri magari yanayotoka Dar hadi Msanga

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI wa Udhibiti Usafiri wa Barabara wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA),Bw. Johansen Kahatano amesema,wamebaini kupitia operesheni zao magari yanayotoka Dar es Salaam kupitia Kisarawe hadi Msanga hayana leseni.

Barabara hiyo ambayo inakadiriwa kuwa na umbali wa kilomita zaidi ya 70 kupitia Maneromango imekuwa kiunganishi muhimu kwa wananchi mbalimbali ambao wamekuwa wakifika au kutoka Dar es Saalaam kwa ajili ya kazi na kujipatia huduma mbalimbali.

Ameyasema hayo Oktoba 19, 2023 katika kikao kazi kati ya LATRA na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Aidha, amesema, mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wameendelea kufanya operesheni za kila wakati katika barabara mbalimbali ikiwemo jijini Dar es Salaam.

"Barabara ya Msanga nikiri tuna changamoto ya magari katika hiyo barabara na kimsingi hayana leseni. Na tumekuwa tukifanya operesheni za kila wakati, hata juzi alifika mtu mmoja analalamika pale ofisini kwetu, gari lake limezuiliwa.

...hawa watu alishakwenda ofisa wetu (LATRA) wakamshambulia, tuna kesi kule polisi katika Kituo cha Stakishari, jeuri tu, juu ya jeruri kwa hiyo tunakamata baadhi ya magari, lakini tunataka waje kuchukua wamiliki wenyewe, tuongee nao ili tuwaeleze madhara ya wanachokifanya.

"Kuna gari moja ambalo mmiliki hakuonekana, anakuja mtu mmoja tu muhuni...muhuni tu, hata jana, juzi alipita pale ofisini tukamwambia hatukupi gari mpaka mmiliki aje, tumweleze kile ambacho sisi tunaona kinamfaa yeye.Kwa hiyo, changamoto ipo, tunaendelea kuyafuatilia magari ambayo hayana leseni,"amesema Kahatano.

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura 413 ili kudhibiti huduma za usafiri ardhini katika Sekta za Reli, Barabara na Waya. Sheria ya LATRA ilifuta Sheria Na. 9 ya mwaka 2001 iliyoanzisha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).

LATRA ilianza kutekeleza rasmi majukumu yake tarehe 29 Aprili, 2019 baada ya Sheria yake kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 358 la tarehe 26 Aprili, 2019.

Aidha, LATRA inasimamia usafiri wa Barabara, Reli na Waya (Cable Car) ambapo kumekuwepo ongezeko la utoaji leseni za mabasi ya abiria (PSV), Malori (GCV), Magari Maalum ya kukodi (Special Hire), Pikipiki za Magurudumu Matatu (Bajaji), Pikipiki za Magurudumu Mawili (Bodaboda), Teksi Mtandao (Ride Hailing) na Teksi Kawaida (Cab).

Katika kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2022/23, idadi ya leseni za usafirishaji ziliongezeka kutoka 230,253 hadi 284,158 sawa na ongezeko la leseni 44,205 ambayo ni ongezeko la asilimia 18.4.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news