Mashirika ya ndege yahakikishiwa usalama nchini

DAR ES SALAAM-Serikali imetoa wito kwa Mashirika ya Ndege ya Ndani na Nje ya Tanzania kutumia Uwanja wa Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kwani ulinzi na usalama kwa ndege, abiria na mizigo umeendelea kuimarishwa kwa kuweka mifumo ya kisasa.

Akizungumza mara baada ya kukagua miundombinu ya Jengo la tatu la Abiria katika kiwanja hicho jijini Dar es Salaam Naibu Waziri, David Kihenzile amesema, uwepo wa usalama umeendelea kuwa na matokeo chanya kwani idadi ya mashirika yanayohudumiwa yamekuwa yakiongezeka ikiwemo Shirika la Ndege la Ufaransa na Shirika la Ndege la Saudia.

“Serikali inayongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kuhakikisha miundombinu ya viwanja inaboresha na mashirika yanayongezeka kwenye viwanja vyetu na hivi karibuni tu hapa tumeongeza mashirika mawili ya nje na moja la ndani kutoa huduma kupitia kiwanja hiki, hii ni hatua kubwa sana,"amesema Naibu Waziri Kihenzile.

Naibu Waziri Kihenzile ameipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA) kwa kuendelea kusimamia viwanja vya ndege na kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa inapotokea changamoto za kiuendeshaji hali inayoongeza imani kwa abiria na mashirika ya ndege.

Aidha, Naibu Waziri Kihenzile ameeleza mipango ya Serikali ni pamoja na kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la pili la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimatiafa cha Julius Nyerere ambapo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria zaidi ya milioni 3 badala ya milioni moja na nusu waliokuwa wakihudumiwa kwa mwaka.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mussa Mbura amemuhakikishia Naibu Waziri Kihenzile kuwa TAA imejipanga kuhakikisha inaboresha zaidi viwanja vya ndege nchini ili kukuza utalii na kuongeza pato la nchi.

Naye Mkurugenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Mhandisi Rehema Myeya amesema, kwa sasa jengo hilo la tatu la abiria linafanya kazi kwa saa 24 na abiria zaidi ya elfu mbili wanaweza kuhudumiwa kwa wakati mmoja.

Naibu Waziri David Kihenzile yuko katika ziara ya siku tano jijini Dar es Salaam ya kukagua miundombinu ya Uchukuzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news