Rais Dkt.Mwinyi:Tutaendelea kudumisha ushirikiano na Oman

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Omar ili kudumisha ushirikiano wa historia uliopo baina ya pande mbili hizo.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Oktoba 10, 2023 Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Ujumbe kutoka Makumbusho ya Taifa ya Oman.

Amesema, Zanzibar na Oman bado zina uhusiano na ushirikiano wa karibu zaidi kutokana na historia za pande mbili hizo, ikiwemo historia, mila na tamaduni zao.

“Kwa sababu hiyo tunafuraha tena kuendelea kushirikiana nanyi na kufanyakazi bega kwa bega kuona namna gani tunaweza kujifunza baina yetu kwa kubadilishana uzoefu, kuchangiana na kubadilishana mawazo na taarifa hivyo tutaendelea kuwa na mwendelezo mzuri wa uhushirikiano wetu,”ameeleza Rais Dkt.Mwinyi.

Akizungumza kwenye maongezi hayo, Mtendaji Mkuu kutoka Makumbusho ya Taifa ya Oman, Jamal Al Moosawi alimweleza Rais Dkt.Mwinyi kwamba, Mamkumbusho ya Taifa ya Oman ni taasisi ya Serikali yenye jukumu la kutunza kumbukumbu za kimkakati za taifa la nchi hiyo kwa muktadha wa kutunza kumbukumbu za diplomasia, urithi wa utamaduni wa nchi hiyo, kuhifadhi masuala ya usalama wa taifa hilo.

Amesema, utamaduni wa kidplomasia ni eneo muhimu linalotunzwa zaidi nakuongeza kuwa makumbusho hiyo ni taasisi pekee inayotunza kumbukumbu za migogoro ya mataifa ya kiarabu ikiwemo Syria, Mogadishu na Somalia.

Naye, Waziri wa Utamaduni na Mambo ya Kale, Simai Muhamed alisema, ushirikiano baina ya Oman na Zanzibar umeendelea kuacha athari kubwa kwa pande mbili hizo ikiwemo mfanano wa mitindo ya tamaduni zao za maisha, vyakula na ustaarabu.

Ujumbe huo wa Makumbusho ya Taifa ya Oman uliongozwa na Mtendaji Mkuu, Jamal Al Moosawi, awali ulitembelea Makumbusho ya Kunduchi jijini Dar es Salaaam ambako imehifadhi magofu ya kale ikiwemo makaburi ya masultani na msikiti uliotumika tangu karne ya 15 hapa Tanzania.

Aidha, ujumbe huo pia uliambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdalla Kilima na Balozi wa mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar, Said Salim Al Sinawi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news