Saudia Arabia yaipongeza Tanzania kwa kudumisha amani, usalama

DAR ES SALAAM-Serikali ya Saudi Arabia imeipongeza Tanzania kwa kuimarisha amani na usalama na pia kupenda wageni wanaoingia nchini kutoka mataifa mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi mpya wa Saudia Arabia nchini, Yahya Ahmed Okeish, wakati alipokuwa akizungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, alipomtembelea ofisini kwake, jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 5, 2023.

Balozi huyo aliyeingia nchini mwezi uliopita, amesema anafurahishwa na usalama wa Tanzania na pia nchi yake ina ushirikiano mzuri na wahistoria wa miaka mingi na nchi yake itaendelea kutoa ushirikiano na kusaidia katika shughuli mbalimbali ya kijamii na maendeleo kwa ujumla.

“Mheshimiwa Waziri nina furaha kuja kuonana na wewe, nimefurahishwa na usalama wa Tanzania, na pia ukarimu wenu wa kupenda wageni waliopo na wanaoingia nchini,” alisema Balozi Okeish.

Pia alisema Serikali ya Saudi Arabia itaendelea kutoa misaada nchini na wana vituo vinavyotoa huduma mbalimbali zinazosaidia kuleta maendeleo nchini, hivyo kupitia uhusiano wa kihistoria kati ya Saudi Arabia wataendelea kutoa huduma pale zitakapohitajika.

Kwa upande wake, Waziri Masauni pia aliipongeza nchi ya Saudi Arabia kwa ushirikiano wake mkubwa kwa Tanzania, na kumkaribisha Balozi huyo kufurahia mambo mazuri yote yaliyopo nchini ikiwemo kujifunza masauala ya utamaduni.

“Mheshimiwa Balozi, nakubaliana na wewe nchi hizi mbili zina ushirikiano mkubwa na pia wa kihistoria, nakukaribisha sana Tanzania, na utajifunza mambo mengi ikiwemo kuhusu utamaduni wetu, pia tunawakaribisha wawekezaji kutoka Saudi Arabia waje nchini kwa kuwa nchi yetu ni salama,” alisema Masauni.

Waziri Masauni alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na Saudi Arabia na pia itaendelea kudumisha amani ambayo iliyopo nchini, na pia aliishukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa misaada mbalimbali ya maendeleo wanayoitoa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news