Serikali yaahidi maboresho zaidi Sekta ya Afya nchini

NJOMBE-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali itaendelea kuchagiza uwekezaji kwenye maeneo yote ya huduma za afya kuanzia ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya, upatikanaji wa vifaa tiba, wataalam pamoja na ujenzi wa viwanda vya bidhaa za afya.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi katika kiwanda cha mipira ya mikono (Gloves) kinachosimamiwa na Bohari ya Dawa (MSD) kilichopo Idofi , Makambako mkoani Njombe. 
 
Amesema Dhamira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. ni kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii kwa kuimarisha afya na kuwezesha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.

Makamu wa Rais amesema serikali itahakikisha kiwanda hicho kinafanya kazi kwa ufanisi kwa kuzingatia faida zake kwa taifa ikiwemo kuongeza upatikanaji wa mipira ya mikono (gloves), kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kupunguza muda mrefu unaotumika katika kuagiza bidhaa hizi kutoka nje ya nchi. Amesema kwa sasa Serikali kwa kupitia MSD inaagiza kutoka nchi mbalimbali duniani, 80% ya dawa, 90% ya vifaa tiba na 100% ya vitendanishi.

Halikadhalika Makamu wa Rais ameagiza kupatikana taarifa ya kina juu ya mitambo mbalimbali iliyohifadhiwa katika moja ya jengo kwenye kiwanda hicho ambayo haijafungwa ili kuanza kutumika tangu mwaka 2021. Aidha amesisitiza kiwanda hicho kuanza uzalishaji ifikapo januari mosi 2024.

Pia Makamu wa Rais ameagiza weledi kuzingatiwa katika uendeshaji wa kiwanda hicho ili kuepuka kuanguka kama ambavyo viwanda vingi vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali vilivyoanguka huko nyuma. 
 
Ameitaka Kampuni Tanzu ya MSD Medipahrm Manufacturing Company Limited kuzingatia misingi ya kibiashara ili iweze kujitegemea katika uzalishaji. 
 
Pia amewasihi watumishi kuwa wazalendo kwa kuweka maslahi ya taifa mbele kuliko biashara zao binafsi ikiwemo biashara za dawa.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito wa kufanyika upembuzi ili kuona namna ambavyo kiwanda hicho kinaweza kutumika kuzalisha bidhaa nyingine zaidi kama vile maji tiba (drip) pamoja na vitendanishi vya maabara kwa kutumia miundombinu iliyopo na hivyo kuongeza tija kwa Taifa.

Mhe. Dkt. Mpango amesisitiza juu ya umuhimu wa kulinda usalama katika Mifumo ya kiwanda hicho kwa kuzingatia viwango ili kuondoa uwezekano wa mifumo hiyo kuhujumiwa na hivyo kuathiri ubora wa bidhaa.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ametembelea na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa katika kiwanda cha Uchambuzi na Ufungashaji Parachichi cha AvoAfrica kilichopo Makambako mkoani Njombe.

Akiwa kiwandani hapo, Makamu wa Rais ameiagiza Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kutatua changamoto wanazopitia wasafirishaji wa zao la parachichi katika mizani ya iliyopo Iringa na Migoli ambayo imetajwa kuwa changamoto katika usafirishaji wa zao hilo. 
 
Pia amewapongeza wawekezaji katika kiwanda hicho na kuwahimiza watanzania hususani vijana kuwekeza katika kilimo cha parachichi kwani zao hilo lenye soko zuri lina fursa katika kuinua uchumi

Makamu wa Rais pia ametembelea na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa katika kiwanda cha uchakataji wa bidhaa za mbao cha Tanganyika Wattle (TANWAT) kilichopo Kibena mkoani Njombe.

Akiwa kiwandani hapo Makamu wa Rais amewaagiza wamiliki wa kiwanda hicho na viwanda vingine nchini kuzingatia maslahi ya wafanyakazi pamoja usalama wao katika maeneo ya kazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news