Tanzania, India kukuza uhusiano wa kimkakati

NEW DELHI-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na India zimekubaliana kukuza uhusiano wao wa kihistoria baina ya mataifa hayo mawili kwa kiwango cha Ushirika wa Kimkakati.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi wakati wakizungumza na Waandishi wa Habari katika Jengo Maalum la kupokelea wageni wa Kitaifa Hyderabad House New Delhi nchini India.

Rais Samia ameyasema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika ziara yake ya kitaifa ya siku tatu nchini India.

Miongoni mwa masuala ambayo viongozi hao wameyawekea msisitizo katika ushirikiano ni pamoja na ulinzi, nishati, kujenga uwezo, usalama wa majini, biashara na uwekezaji.

Hadi kufika mwaka 2022, kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili ulifikia dola za Kimarekani bilioni 3.1, hivyo kuifanya India kuwa mshirika wa tatu kwa ukubwa katika biashara na mwekezaji wa tano kwa ukubwa nchini Tanzania.

Wakati huo huo, nchi hizo mbili zimetia saini hati za makubaliano 14 na mkataba mmoja, ambapo hati 10 zimehusisha taasisi za serikali na mitano ni za sekta binafsi.

Mbali na kuwa tayari India inaisaidia Tanzania katika masuala ya ubobezi wa kupandikiza figo na uboho (bone marrow), pia viongozi hao wamejadili namna ya kuanzisha kituo cha dawa asilia.

Rais Samia ameshukuru pia kwa kuanzishwa kampasi ya kwanza ya chuo cha IIT nje ya India chenye hadhi ya juu katika masuala ya teknolojia visiwani Zanzibar kitakachowanufaisha wanafunzi mbalimbali, siyo tu wa Tanzania ila hata nje ya mipaka.

Masuala mengine yaliojadiliwa katika ziara ya Rais Samia ni pamoja na usalama wa mitandao, kushirikisha vijana hasa kupitia vyuo vya VETA, kutoa mafunzo kwa wahandisi wa madini, kushirikiana kwenye kilimo na miradi ya maji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news