TUAMUE KUTUMIA, HII GESI ASILIA

NA LWAGA MWAMBANDE

OKTOBA 18, 2023 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kuweka kipaumbele katika kusambaza Vituo vya Nishati ya Gesi Iliyoshindiliwa (CNG) inayotumika katika kuendesha mitambo na magari nchini ili kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa mafuta pale zinapotokea.

Ushauri huo umetolewa jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Mathayo David wakati kamati hiyo ilipopokea taarifa ya Wizara ya Nishati, kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi wa kuanzisha vituo hivyo.

Vile vile, Mheshimiwa Mathayo ameipongeza Serikali kwa mikakati mizuri ya uanzishwaji wa karakana za kubadili mifumo ya matumizi kutoka kwenye mafuta na kwenda kwenye gesi asilia kwenye magari hali inayochochea matumizi ya gesi asilia nchini kwa wingi.

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande licha ya kuipongeza kamati kwa ushauri huo, pia amesisitiza kuwa, matumizi ya gesi asilia licha ya kuwa rafiki kwa mazingira vivyo hivyo ni rahisi kwa uendeshaji wa vyombo vya moto, Endelea;


1.Ni mambo ya kukazia, hapa kwetu Tanzania,
Tuamue kutumia, hii gesi asilia,
Mungu alotupatia, ni nyingi imejazia,
Kamati yetu ya Bunge, asante kwa ushauri.

2. Kamati Nishati nia, hili mmeshindilia
Kwa Njuga kulivalia, gesi yetu kutumia,
Pesa kujizungushia, hapa ndani kusalia,
Kamati yetu ya Bunge, asante kwa ushauri.

3.Kusini imejazia, Dasalamu yafikia,
Mitambo kuitumia, na hata magari pia,
Yaweza tupunguzia, dola tunazowania,
Kamati yetu ya Bunge, asante kwa ushauri.

4.Gesi wanashindilia, viwanda twazalishia,
Shida tunayopitia, dola kuzifukuzia,
Inaweza kuishia, zaidi tukitumia,
Kamati yetu ya Bunge, asante kwa ushauri.

5.Kama ukifwatilia, Dar es Salaam pitia,
Wapo gesi watumia, tena wanafurahia,
Changamoto yasalia, vituo kuvifikia,
Kamati yetu ya Bunge, asante kwa ushauri.

6.Ujuzi umetimia, gari kubadilishia,
Gesi iweze tumia, sawa na mafuta pia,
Yale yaliyosalia, gesi kutusambazia,
Kamati yetu ya Bunge, asante kwa ushauri.

7.Serikali yetu pia, imetuthibitishia,
Mkazo itatilia, gesi yetu kutumia,
Hilo tunafurahia, kazi tunasubiria,
Kamati yetu ya Bunge, asante kwa ushauri.

8.Fursa inatujia, bei kujipunguzia,
Hii gesi asilia, shilingi tunatumia,
Dola tunazolilia, hatutazihitajia,
Kamati yetu ya Bunge, asante kwa ushauri.

9.Faida nyingi sikia, kwa dola Watanzania,
Gesi hii asilia, hapa twajichukulia,
Vituo jianzishia, hamasika nakwambia,
Kamati yetu ya Bunge, asante kwa ushauri.

10.Wenye magari sikia, tumia kufurahia,
Ama gesi asilia, au mafuta sikia,
Ila kinachovutia, pesa unazotumia,
Kamati yetu ya Bunge, asante kwa ushauri.

11. Bei gesi asilia, nusu mafuta sikia,
Lita unajipatia, mbali unasafiria,
Tena bila kuchangia, anga kutuchafulia,
Kamati yetu ya Bunge, asante kwa ushauri.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news