Waziri Masauni azindua zoezi la ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa

NA FRESHA KINASA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Yusuph Masauni amesema kuwa, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mtanzania mwenye sifa anapata kitambulisho cha Taifa (NIDA), kwani Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imejipanga vyema kutekeleza jambo hilo kwa ufanisi.

Waziri Masauni ameyasema hayo wakati wa Uzinduzi wa Ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa umma Oktoba 12, 2023 Mjini Musoma mkoani Mara. Ambapo pamoja na mambo mengi amesema kuwa, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inapaswa kuhakikisha na kubaini wote ambao wana sifa stahiki wanapata kwa kuzingatia usalama wa nchi.

Amesema kuwa, madeni ambayo mzabuni alikuwa akiidai serikali yatari alilipwa na pia tatizo la kadi ghafi ambalo lilikuwepo limepatiwa ufumbuzi kwa Serikali kutoa shilingi Bilioni 42.5 ambazo zitatatua changamoto hiyo, huku akisema thamani ya kitambulisho hicho kwa sasa ni muhimu katika matumizi mbalimbali hivyo wananchi wanapaswa kuvitunza.

Pia, Waziri Masauni ameitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) isitegemee mtandao mmoja na kwamba jambo hilo lisiwe sababu ya kudhorotesha majukumu yake kwani dhamira ya Serikali ni kuona kwamba utekelezaji wa zoezi unakuwa na ufanisi na weledi.

Aidha, Waziri Masauni amewataka Watanzania kufika katika Ofisi za serikali za mitaa na vijiji kuchukua vitambulisho vyao na kwa wale ambao bado serikali itahakikisha wanavipata kwa muda mfupi ujao baada ya kuzalishwa.

Ambapo kwa Mkoa wa Mara wenye Namba za NIDA ni Wananchi 744, 872 na ambao Wana Kadi mpaka Sasa ni 26,435. Hivyo Wananchi wengine watapata Vitambulisho vyao baada ya uzinduzi huo kwa kwenda Ofisi za serikali za mitaa na vijiji kuchukua.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Said Mtanda amewataka viongozi waliopewa dhamana ya kugawa vitambulisho hivyo mkoani humo kuvigawa kwa haki bila kuwatoza fedha wananchi kwani vitambulisho hivyo ni bure.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),Mhandisi Ismail Lumatira amesema kuwa, hali ya usajili na utambuzi wa watu linaendelea kufanywa vyema na Mamlaka hiyo.

"Tangu kuanza kwa utekelezaji wake mwaka 2012 mpaka mwishoni mwa Septemba 2023 jumla ya watu milioni 24, 145, 044, idadi hii ya watu waliosajiliwa ni sawa na asilimia 76.7 ya watu milioni 31,477, 938, wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea kulingana na sensa ya watu ma makazi ya mwaka 2022," amesema na kuongeza kuwa.

"Namba za Utambulisho wa taifa (NISs) zilizozalishwa tangu 2012 kufikia milioni 20,437,372, sawa na asilimia 84.6 ya watu waliosajiliwa (NIS) zimegawiwa kwa wananchi ili wazitumie kwa shughuli mbalimbali.

"Upande wa Vitambulisho vya Taifa hadi kufikia Septemba 2023 NIDA imefanikiwa kuzalisha vitambulisho milioni 14,490, 390, tangu 2012," amesema na kubainisha kuwa,

"Hiyo ni sawa na asilimia 70.9 ya namba za Utambulisho milioni 20, 365,783 zilizozalishwa pia imesambaza kwa wananchi vitambulisho milioni 12, 646, 491 kati ya vitambulisho vilivyozalishwa," amesema Mhandisi Lumatira.

Aidha, amebainisha kwamba,Serikali ya Awamu ya Sita imeweza kutoa fedha shilingi bilioni 42.5 zilizowezesha kununulia kadi ghafi milioni 13,514, 251, zitakazotosheleza kuzalishwa kwa vitambulisho vya watu wote wenye namba za utambulisho.

Amesema, mpaka sasa tayari NIDA imeshapokea kadi ghafi milioni 6, 272, 836, kutoka kwa mzabuni na matarajio kufikia Desemba, mwaka huu watakuwa wanepokea kadi ghafi milioni 7, 241, 145 zilizosalia.

Ameongeza kuwa, kwa mwaka 2023/ 2024 mamlaka imeandaa mpango mkakati wa kuhakikisha mara tu vitambulisho vinapozalishwa na kusambazwa na kugawiwa kwa wananchi, hivyo hadi kufikia mwaka 2024 vitambulisho milioni 10 vinatarajiwa kusambazwa na kugawiwa kwa wananchi. Huku akisema serikali imadhamiria kujenga kiwanda cha kuzalisha kadi ghafi hapa nchini na mchakato wa awali umeanza.

"Mamlaka imekuwa ikigawa kwa njia tatu,wananchi kwenda Ofisi za Usajili za Mamlaka kuchukua kitambulisho,ugawaji wa jumla kwenda kwa watendaji wa serikali za mitaa na vijiji kwa Tanzania bara na Ofisi za Shehia kwa Zanzibar ambazo hutumika katika zoezi la Ugawaji wa Vitambulisho na Ugawaji kwa umma ambao umekuwa ukiendeshwa na watumishi wa mamlaka kwa kushirikiana na TAMISEMI na Idara Maalumu za serikali ya Zanzibar kwa kwenda kuendesha maeneo ya makazi," amesema Mhandisi Lumatira.

Nao baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Musoma wakizungumza na DIRAMAKINI wameiomba serikali kuongeza kasi ya uzalishaji wa vitambulisho hivyo wakidai baadhi ya taasisi ambazo wamekuwa wakienda kupata huduma mbalimbali wamekuwa wakiombwa vitambulisho na wanaposema wana Namba ya NIDA baadhi ya watoa huduma hutoa huduma kwa shingo upande.

"Nilienda taasisi moja ya fedha naihifadhi, nikaombwa kitambulisho nilipowapa Namba ya NIDA wakasema wanahitaji kitambulisho mkononi sio namba, mmoja wa watumishi katika taasisi ile akanihurumia akaniprintia mtandaoni.

"Lakini akasema siku nyingine niende na kitambulisho nawapa usumbufu bila huduma ya yule ndugu nisingepata huduma ni vyema serikali izalishe kwa kasi wananchi tuvipate wote,"amesema Rhoda Jackson mkazi wa Musoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news