Haya hapa, mahojiano kati ya Rais Dkt.Mwinyi na Benny Mwaipaja kuelekea IDA20 Mid-Term Review

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Tathimini ya Muda wa Kati wa Mzunguko wa 20 wa Benki ya Dunia (IDA20 Mid-Term Review) utakaofanyika Zanzibar kuanzia Desemba 6 hadi 8, 2023.

Amesema, ugeni huo utarajie kushuhudia maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii yaliyofikiwa kupitia mikopo nafuu na misaada kutoka Benki ya Dunia.

Kupitia mkutano huo ambao unatarajia kuwashirikisha wajumbe zaidi ya 300 kutoka mataifa takribani 100 duniani, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amewataka wananchi kuchangamkia fursa za ugeni huo katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametoa wito huo baada ya kufanya mahojiano na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja ikiwa ni maandalizi ya kuelekea katika mkutano huo. Mahojiano yalikuwa hivi;

Benny Mwaipaja:Mheshimiwa Rais hongera sana kwa kutimiza miaka mitatu ya uongozi wako hapa Zanzibar, lakini pia tumeona maendeleo makubwa ambayo umeyafanya na wananchi kwa ujumla wanastahili kukupa maua yako, kwamba mambo mengi yamefanyika na mambo mengi tunayaona kwa macho yetu. Waswahili wanasema asiye na macho haambiwi tazama.

Lakini, kilichotukutanisha hapa sasa kwa muda huu ni kwamba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, itakuwa na ugeni mkubwa sana wa Kimataifa ambao utakuwepo hapa Zanzibar kuanzia tarehe 3, lakini mkutano wenyewe unaanza tarehe 6 mpaka tarehe 8 (Desemba).

Ni mkutano mkubwa sana, unawashirikisha wajumbe zaidi ya 300 ambao ni wanufaika kutoka nchi 75, wanachama 75 ambao ni wanufaika wa IDA, mfuko ambao unahusika na kutoa misaada na mikopo kwa nchi ambazo zinaendelea. Zanzibar na Tanzania kwa ujumla mmejiandaaje kupokea ugeni wa namna hii?.

Rais Dkt.Mwinyi:Kwanza niseme,tunashukuru sana kwa Zanzibar kupata fursa ya kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huu, wa nchi nyingi ambazo zinakuja hapa Zanzibar kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huu muhimu sana, katika maendeleo ya nchi zetu.

Sisi, kama Serikali tumejipanga vizuri kuupokea ugeni huu mkubwa, na kwa kweli unatupa heshima kubwa ya kwamba kwanza tunakaribisha watu kadhaa ambao kwa upande wetu pia utakuwa na manufaa kiutalii.

Wakati huo huo, tunasajihisha sekta binafsi nao wawe tayari kuupokea ugeni huu, waweze kutoa huduma mbalimbali, waweze kunufaika nao.

Benny Mwaipaja:Tanzania katika ripoti ya miaka sita imenufaika na mikopo nafuu kutoka Benki ya Dunia ambayo inafikia takribani dola bilioni 8.3, sawa na shilingi trilioni 20, Zanzibar iko humo ndani mnufaika, unaweza kuelezeaje manufaa ya Benki ya Dunia kwa Zanzibar na Tanzania?.

Rais Dkt.Mwinyi: Lazima nikiri kwamba moja katika wadau wakubwa wa maendeleo kwa Tanzania na Zanzibar ni Benki ya Dunia, na kama ulivyosema fedha nyingi sana zimetolewa na hapa Zanzibar tumekuwa ni sehemu ya kupokea fedha hizo na baadhi ikiwa ni misaada na baadhi ikiwa ni mikopo.

Na tumeweza kunufaika nayo na kufanya miradi mikubwa sana ya maendeleo, kwa uchache tu niseme miradi kadhaa ambayo aidha imeshafanyika na mingine inaendelea kufanyika na bado ipo mingine ambayo ipo katika hatua za upangaji.Kwa mfano, kuna mradi ambao tunauita...Endelea kutazama video chini;


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news