Maafisa Ugani mkoani Mara watakiwa kuwafikia wakulima

NA FRESHA KINASA

SERIKALI ya Mkoa wa Mara imewataka Maafisa Ugani mkoani humo kuwafikia Wakulima katika maeneo yao kuwapa mbinu na elimu ya Kilimo mseto na Kilimo hifadhi kusudi wazalishe kwa tija.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Said Mtanda ameyasema hayo leo Novemba 18, 2023 kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Jumaa Chikoka wakati akihitimisha Maonesho ya Nane ya Kilimo Mseto na Uhifadhi ambayo yameendana sambamba na maadhimisho ya miaka 40 ya Shirika la Vi-Agforestry katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Maonesho hayo yamefanyika katika viwanja vya AICT Bweri Mjini Musoma mkoani humo kuanzia Novemba 16, 2023 hadi Novemba 18, 2023. Ambapo yalizinduliwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena kwa Niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Riziki Shemdoe.

Mtanda amesema kuwa, wakulima wanahitaji elimu, ujuzi na utaalamu kusudi wazalishe kwa tija katika kukabiliana na changamoto za kimazingira na mabadiliko ya tabia nchi. Hivyo, Maafisa Ugani katika Mkoa wa Mara watekeleze jukumu hilo kwa ufanisi.

Aidha, Mtanda amewataka Viongozi wa Mkoa wa Mara kuhakikisha miti yote iliyopandwa katika taasisi mbalimbali za umma wanaisimamia ikue pamoja na kuhamasisha Wananchi kupanda miti katika maeneo yao na kuitunza sambamba na kuhifadhi mazingira.

Amesema kuwa, Mkoa wa Mara umeendelea kuweka mazingira mazuri na wezeshi kwa ajili ya Kilimo, ambapo amesema mkoa upo tayari kushirikiana na wadau wa Kilimo kuhakikisha unazalisha Chakula cha kutosha na Wananchi kujipatia maendeleo.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Mkoa wa Mara inaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na shiraka hilo katika kuwajengea uwezo wakulima, uhifadhi wa mazingira na kuwaleta pamoja wadau kushiriki katika sekta ya Kilimo.

Kwa upande wake Lidia Kabaka kutoka Shirika la BUFADESO la Wilaya ya Bunda linalojishughulisha na masuala ya kilimo akisoma mapendekezo ya wakulima amesema Serikali unawajibu wa kuongeza wigo kufuatilia wakulima ili kujua mwenendo wao, na pia Serikali ione umuhimu wa uzalishaji mashamba darasa kwa ajili ya wakulima kupata elimu ya kilimo bora.

Pia,amesema Serikali ihamasishe Kilimo endelevu na utunzaji mazingira katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Wakulima walioshirki katika maonesho hayo, wamesema kuwa wamejifunza mambo mbalimbali muhimu yatakayowasaidia kufanya shughuli za kilimo na kuzingatia Kilimo bora katika maeneo yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news