Wapigakura wasajiliwe kidigitali

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba ameshauri kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iangalie namna ambavyo itakuja na mfumo wa kusajili wapigakura nchini kidigitali.

Kibamba ambaye pia ni mchambuzi mbobezi katika masuala ya kisiasa Kitaifa na Kimataifa ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanahabari, ikiwa Watanzania wanatarajia mwaka kesho kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa kabla ya kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Amesema kuwa, "Tume ya Taifa ya Uchaguzi iingie kidigitali, ianzishe mfumo ambao kwa mfano vijana wanaotimiza miaka 18, akitimiza miaka 18 anaweza kujisajili siku hiyo hiyo kuwa mpiga kura, unafanyaje? Unaanzishwa mfumo wa kidigitali ambapo tume itaandaa App.

"Sasa hayo ni mambo ya kidigitali ya vijana hayo, itaandaa App (programu tumishi kupitia simu janja) mtu anaweza kujisajili mwenyewe akatuma taarifa kama ambavyo watu wanajisajili kufungua akaunti ya benki sasa hivi.

"Unatuma zile taarifa, zile taarifa zikifika Tume ya Taifa ya Uchaguzi, tume inazihakiki, inazikagua ikiona zipo sahihi inatuma kwa yule mtu aliyejiandikisha, namba ya mpiga kura, unatumiwa namba kama NIDA wanavyofanya.

"Wanakutumia ukishajiandikisha namba ya NIDA unasubiria kitambulisho kitaletwa siku ambayo tume sasa itakuwa inapita,"amefafanua Kibamba.

Mbali na hayo, Kibamba amesema wamefanya utafiti ni kwa namna gani ambavyo Watanzania hususani vijana wanaotimiza miaka 18, lakini hawana simu janja watakavyojiandikisha na kupata ufumbuzi.

"Tumefanya utafiti, je? Watanzania wanajiuliza mtu ambaye ametimiza miaka 18, lakini hana simu inayoruhusu kufungua App,afanyeje? Au anayo simu, lakini hajui namna ya kuweza kutumia App ya kidigitali.

"Likaja suluhisho lingine, kuna mapendekezo ambayo timu yangu imepata kwamba, kunaweza kukaanzishwa katika huu mfumo wa kujisajili wa mpiga kura, ukaanzishwa utaratibu wa mawakala wa usajili wa wapigakura.

"Mawakala hawa watafanana na mawakala wa TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania) ambao watu wengi hawajui kama wale ni mawakala wa TCRA,lakini mnawaona watu wameweka pale miamvuli wanasema tunasajili laini.

"Sheria itaelekeza kwamba, kutakuwa na mfumo wa kujisajili mwenyewe na mfumo wa mawakala wa kusajili wapiga kura ambao mawakala hao watakuwa wanamsajili mtu.

"Na bahati nzuri wana vifaa vyote, na hao mawakala wanaweza wakawa ni wale wale ambao wanasajili laini, wakaongezewa majukumu tu, wakawa wana uwezo wa kumsajili mtu wakachukua alama za vidole, wakampiga picha, wakatuma zile taarifa kimtandao kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kama sawa sawa na yule aliyejisajili mwenyewe.

"Wakasubiri mpaka tume iweze kuhakiki zile taarifa itume namba ya kitambulisho, kwa hiyo yule mteja aliyejiandikisha atakuwa anakuja kuangalia taarifa zake pale pale alipojiandikishia ambapo labda ni kijijini kwako pale pale, au ni kwenye mtaa wako ule ule kiasi ambacho tutakuwa tumerahisisha.

"Lengo ni mfumo wa kuandikisha wapigakura urahisishwe, uwe mwepesi na wapiga kura wengi waweze kujiandikisha.

"Si vizuri hata kidogo, kwa nchi kama Tanzania kwa sensa (Sensa ya Watu na Makazi 2022) iliyopita yenye Watanzania milioni 62, kwamba unakuta wapiga kura wanajiandikisha chini ya milioni 30.

"Yaani chini ya nusu ya Watanzania waliojiandikisha, kwa sababu gani? Kwa hiyo ugumu wa kujiandikisha umekuwa ni kichocheo cha Watanzania wengi kuamua kutokupiga kura,"amesisitiza Kibamba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news