Watoto 79,000 kupatiwa chanjo ya kichocho Kasulu

NA RESPICE SWETU

JUMLA ya watoto elfu sabini na tisa wenye umri wa miaka mitano hadi miaka kumi na nne, wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa kichocho na minyoo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Akizungumza wakati wa kikao cha maandalizi ya utoaji wa chanjo hiyo, mratibu wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Hussein Pengu amesema, chanjo hizo zitawahusu watoto wenye umri wa miaka mitano hadi miaka kumi na nne walio shuleni na walio nje ya shule.

Ameongeza kuwa, ili kupata takwimu sahihi za watoto watakaopatiwa chanjo, utaratibu wa kuwaingiza katika rejesta maalumu utatumika ili kuwatambulisha watoto waliopatiwa chanzo hizo walio shuleni na walio nje ya mfumo wa shule.

"Kutakuwepo na rejesta za aina mbili wakati wa kutoa chanjo hizo, moja itatumika kwa ajili ya watoto walio shuleni na ya pili itatumika kwa ajili ya watoto walio nje ya shule,"amesema.

Pengu amevitaja vituo vitakavyohusika na utoaji wa chanjo hizo kuwa ni shule za msingi na kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Zoezi hilo lililopangwa kufanyika Novemba 24, linaratibiwa kwa ushirikiano wa idara ya afya na idara ya elimu ya halmashauri ya wilaya ya Kasulu,

Ili kufanikisha zoezi hilo, afisaelimu msingi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Elestina Chanafi, amewataka walimu kutoa ushirikiano wa kutosha kwenye zoezi hilo.

"Kama ilivyo ada hasa katika utoaji wa dawa za kichocho, watoto watatakiwa kula shuleni, kila shule inatakiwa kuandaa chakula cha watoto kulingana na mazingira yake,"amesema.

Sanjari na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, zoezi hilo linatekelezwa katika halmashauri zote za mkoa wa Kigoma.

Chanjo hiyo pia inafanyika kwenye halmashauri za mikoa ya Mwanza na Kagera zilizo na kiwango kikubwa cha maambukizi ya magonjwa hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news