MAAFA KATESH:Fahamu kwa nini bosi wa UWT na msafara wake walianza kulia

MANYARA-Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda na msafara alioambata nao wamejikuta katika simanzi nzito mara baada ya kumuona mama aliyejifungua saa chache mara baada ya kuokolewa kwenye tope ambalo lilikuwa limemuenea mwili mzima na kumsomba mita kadhaa.
Akizungumza alipomtembelea mwanamke huyo katika Kituo cha Afya Gendabi mahali ambapo ndipo kulikuwa na maafa makubwa kufuatia mafuriko yaliyotokea mara baada ya Mlima Hanang' kuporomoka, Chatanda alisema;

"Nimeshindwa kujizuia mimi kama mama nikajikuta nalia kwa uchungu kuona mwanamama huyu ambaye alisombwa na tope na kuweza kuokolewa kwenye tope hilo na kufikishwa hospitali masaa mawili baadaye kujifungua salama mtoto wa kiume kwa kweli nimelia kwa uchungu baada ya kusikiliza simulizi za Mama huyu.

"Namna alivyohangaika kuokoa watoto wake wawili na huku mjamzito wa miezi tisa hakika hakuna kama Mama.

"Namshukuru sana Mungu kutenda maajabu na kumuwezesha Mama huyu kujifungua salama na mtoto yupo salama na ameitwa Mussa ."

Mwenyekiti huyo amesema, jumuiya itafanya jitihada kuhakikisha wanamuongezea mahitaji ya kutosha

mama huyo ambaye kwa sasa yeye na familia wanalala hospitali kutokana na kukosa makazi.

Ni baada ya makazi yao kuharibiwa vibaya kutokana na mafuriko ya matope yaliyoikumba baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Hanang'.

Janga hilo lilitokea Desemba 3, 2023 kwenye mji mdogo wa Katesh na vitongoji vya karibu vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay na Sebasi, wilayani Hanangi mkoani Manyara.

Aidha, maafa hayo yalifuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku Jumamosi, tarehe 02 Desemba, 2023 na hatimaye kufuatiwa na tukio hilo alfajiri ya Jumapili, tarehe 3 Desemba, 2023 majira ya saa 11:30.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news