MAAFA KATESH:Serikali yatoa taarifa ya maendeleo ya hali ilivyo

MANYARA-Desemba 5,2023 majira ya saa 9:00 alasiri Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw.Mobhare Matinyi akiwa Katesh ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Hanang' mkoani Manyara ametoa taarifa ifuatayo;

UTANGULIZI

Ifuatayo ni taarifa fupi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya leo tarehe 05 Desemba, 2023, kuhusu maendeleo ya kazi ya uokoaji wa waathirika na mali pamoja na utafutaji wa miili kufuatia janga la maporomoko ya tope, maji, mawe na magogo kutoka mlima Hanang.

Janga hili lilitokea kwenye mji mdogo wa Katesh na vitongoji vya karibu vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay na Sebasi, wilayani Hanang, mkoani Manyara.

Maafa haya yalifuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku Jumamosi, tarehe 02 Desemba, 2023; na hatimaye kufuatiwa na tukio hili alfajiri ya Jumapili, tarehe 03 Desemba, 2023, majira ya saa 11:30.

Kamati ya Maafa ya Wilaya pamoja na ya Mkoa wa Manyara chini ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Queen Sendiga, zote ziliitikia kwa haraka asubuhi hiyo hiyo na kuanza kulishughulikia janga hilo.

Aidha, mikoa jirani ya Arusha, Singida na Dodoma nayo iliitikia kwa haraka na kuleta wataalamu wa tiba 15 na magari ya kubebea wagonjwa. Baadaye mkoa wa Singida pia ulitoa majeneza yaliyosaidia kutunzia miili ya marehemu.

Aidha, Kamati ya Maafa ya Kitaifa chini ya uratibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama, ilianza kazi mara moja siku ya tukio ikiwa na Kamati ya Wataalamu inayoongozwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi.

Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu Kamati ya Kitaifa ambayo hadi sasa inajumuisha wizara za kisekta kama ifuatavyo: Ulinzi na Jeshi la Kujenga; Mambo ya Ndani ya Nchi; Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Madini; Afya; Kilimo; Nishati; Ardhi na Makazi; Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum; Maliasili na Utalii; na Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Pamoja na kamati hii ya wizara za kisekta lakini pia kuna timu ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Taifa inayojumuisha wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama vikiongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JTWZ),Jeshi la Polisi Tanzania, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Magereza na Jeshi la Uhamiaji.

Kamati hii imetoa askari zaidi ya 1,283 na hali kadhalika imeungwa mkono pia na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ambalo nalo pia limeleta askari wake.

ZIARA YA WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, jana tarehe 04 Desemba, 2023, alikuja mjini Katesh kujionea hali ilivyo na kupokea taarifa ya awali kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista
Mhagama, aliyekuwa akiongoza timu ya Mawaziri inayounda Kamati ya Kitaifa.

Waziri Mkuu alipata fursa ya kuzuru maeneo yaliyoathirika kwa kutumia mjini Katesh na kisha kwenda kwa helikopta kwenye vijiji vilivyoathirika ambapo alipofika Gendabi alishuka na kuwatembelea wananchi walionusurika na janga
hili, kuzungumza nao na kuwapa pole akiwa na Mawaziri, uongozi wa mkoa pamoja na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

RAIS KUKATISHA ZIARA YAKE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekatisha ziara yake kwenye Mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP28) unaoendelea Dubai, Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE).

Baadaye leo jioni mara baada ya Mhe. Rais kuwasili nchini,Waziri Mkuu Majaliwa atampatia taarifa rasmi ya tukio hili na juhudi za serikali za uokoaji na uopoaji pamoja na huduma zinazoendelea hivi sasa.

VIFO NA MAJERUHI

Hadi kufikia leo tarehe 05 Desemba, 2013, saa 1:00 asubuhi, jumla ya majeruhi 117 walikuwa wameshapokelewa katika Kituo cha Afya Gendabi, Hospitali ya Wilaya ya Hanang (Tumaini) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.

Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakishirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama Desemba 4, 2023 kubeba miili iliyoopolewa baada ya kunasa katika tope kutokana na mvua kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko Wilaya ya Hanang; mkoani Manyara.

Kati ya majeruhi hawa 18 hawakuwa na hali nzuri na walihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kwa matibabu zaidi ambapo mmoja (1) kati yao alifariki dunia siku moja baadaye, tarehe 04 Desemba, 2023, saa 4:00 usiku.

Majeruhi wengine 17 bado wanaendelea na matibabu hospitali hapo. Majeruhi wengine 74 (ambao hawakupelekwa hospitali ya mkoa) bado wanaendelea kupata huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang (Tumaini) na Kituo cha Afya Gendabi mjini Katesh.

Na majeruhi waliotibiwa na kupata nafuu hatimaye kuruhusiwa kurejea nyumbani ni 25.

Mchanganuo wa majeruhi 117 hadi kufikia asubuhi 05/12/2023 ni: Watu wazima 61: (Wanaume 30; wanawake 31).
Watoto ni 56: (Wanaume 27; wanawake 29).

Jumla ya miili 65 ilipokelewa na kuhifadhiwa katika Kituo cha Afya Simbay, Kituo cha Afya Magugu, Hospitali ya Dareda, Hospitali ya Mji wa Babati, Hospitali ya Wilaya ya Hanang (Tumaini), na Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Manyara.

Mchanganuo wa vifo 65 vya marehemu waliopokelewa hadi kufikia asubuhi 05/12/2023 ni:
Watu wazima 41: (Wanaume 15; wanawake 26). Watoto ni 24: (Wanaume 10; wanawake 14).

KAMBI ZA WAATHIIRKA

Hadi sasa kuna jumla ya waathirika 190 kama ifuatavyo:
- Shule ya Sekondari Katesh = 118 (Wanaume 46 na Wanawake 72).
- Shule ya Msingi Gendabi = 66 (Wanaume 40 na Wanawake; 14
Watoto wa Kiume 4 na Watoto wa Kike 8).
- Shule ya Msingi Ganana = 6 (Wanaume 2 na Wanawake 4) – Hawa wanatarajiwa kuhamishiwa kwenye kituo cha Shule ya Sekondari Katesh kwa ajili ya kuboresha ufanisi wa huduma.

JUHUDI ZA SERIKALI HADI SASA:

Aidha, kwa maelekezo ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhusu Hassan, Serikali inaendelea kulishughulikia janga hili kwa kutumia wizara za kisekta na vyombo vya dola kama ifuatavyo:

- Imeweka kambi tatu kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa janga hili katika shule tatu ikiwapatia chakula, matibabu na malazi.

- Kuandaa na kugharamia mazishi ya watu wote waliopoteza maisha. Wananchi wameendelea kuchukua maiti za wapendwa wao ambapo hadi kufikia asubuhi leo maiti 60 zilikuwa zimeshachukuliwa na tano (5) zilikuwa hazijatambuliwa.
- Kutoa matibabu ya bure kwa waathirika wote.
- Kuwapatia chakula na malazi ya dharura manusura waliopoteza makazi
yao na majeruhi waliotoka hospitali.
- Kuondoa tope lililojaa mitaani na barabarani katika mji mdogo wa Katesh
– kazi iliyoanza siku ya tukio na kuwezesha barabara kuu ya kutoka
Babati kwenda Singida kufunguka.
- Kufukua mali na nyumba zilizoma kwenye tope na kutafuta iwapo bado
kuna miili.
- Kurejesha huduma za umeme, maji, mawasiliano na kuthibiti usalama.
- Kuondoa wananchi wengine ambao nyumba zao zimeathirika na waliopo kwenye njia ya maji kutoka milimani ili kuwaepusha na lolote linaloweza kutokea katika siku chache zijazo kwani mvua bado zinaendelea nchini.

MADHARA KWA UJUMLA

Kwa ujumla kaya 1,150 zenye watu 5,600 zimepoteza makaazi yake katika mji mdogo wa Katesh na vitongoji vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay na Sebasi.

CHANZO

- Ni kumeguka kwa sehemu ya mlima Hanang yenye miamba dhoofu iliyonyoya maji ya mvua na kuporomoka (landslide) na hivyo kutengeneza tope (mudflow).

- Sehemu ilinyonya maji ilizua mgandamizo na sehemu ya mlima ikashindwa kuhimili mgandamizo na hivyo kusababisha kumegeka kwa sehemu hiyo na kutengeneza tope ambalo ndilo lilianza kuporomoka kufuata mkondo wa mto Jorodom huku likizoa mawe na miti na kwenda kupiga makazi ya binadamu yaliyokuwa pembezoni mwa mto.

-Mlima Hanang umeundwa na miamba laini ijulikanayo kama volcanic sediments (chembechembe za mchanga uliotokana na kivolkano).
- Serikali imefuatilia taarifa za matetemeko kuanzia Septemba 2023 hadi siku ya tukio na hakukuwa na tetemeko lolote wala mlipuko wa volkano.
- Uchunguzi ulifanywa kwa kupita kwa miguu, helikopta ili kufanya uchunguzi huo.

MAHITAJI
Serikali inatoa wito kwa kampuni, mashirika, taasisi za umma na binafsi, wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kujitolea kwa hali na mali ili kuwaisaidia wenzetu waliopatwa na janga hili. Bado tunahitaji vyakula, vifaa, mitambo,
madawa na mahitaji mengine.

Kwa misaada ya fedha, Waziri Mkuu ameelekeza, kwamba mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022 na kanuni zake za mwaka 2022, fedha zote zitumwe kwenye akaunti ya Kamati ya Maafa ya Taifa:

National Disaster Management Fund Electronic Account 9921151001 kwa kuandika neno MAAFA HANANG. Benki yoyote ndani na nje ya nchi inaweza kupokea fedha kupitia akaunti hii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news