RC Chalamila ahamasisha uwekezaji, matumizi ya Kiswahili barani Afrika

NA GODFREY NNKO

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila ameyakaribisha mataifa ya Afrika kuwekeza hapa nchini huku akiwahamasisha wageni kuendelea kujifunza lugha ya Kiswahili ambayo inaendelea kutumiwa na mamilioni ya watu ndani na nje ya Tanzania.

Hayo ameyasema leo Desemba 6, 2023 wakati akitoa salamu za Mkoa wa Dar es Salaam katika ufunguzi wa Kongamano la Wanawake katika Biashara kupitia Ukanda huru wa Biashara barani Afrika (AfCTA).

Kongamano hilo la siku tatu ambalo linaendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere limezinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

"Dar es Salaam ni mkoa wenye amani ya kutosha, tuna idadi ya watu si chini ya milioni tano katika jiji letu. Kwa mantiki hiyo ni mkoa mkubwa sana, na una fursa za uwekezaji za kutosha,

"Kwa hiyo,wageni ambao mmetoka sehemu za mbali karibuni sana Mkoa wa Dar es Salaam ili muweze kuwekeza.

"Na Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla, tunatumia Kiswahili kama lugha ya Taifa, nitumie nafasi hii pia kuwahamasisha wageni wote mliokuja hapa kwamba mnapoondoka hapa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla angalau anzeni kujifunza lugha ya Kiswahili.

"Kwa sababu ni lugha rasmi sasa katika Afrika na Duniani kwa ujumla, kwa hiyo niwaombe sana mjifunze lugha ya Kiswahili ili muweze kuwasiliana na ndugu zenu, mpate uelewa wa kufahamnu kilichoko Tanzania kwa nafasi yako au kwa faida ya hapo baadae."

Vile vile, Mheshimiwa Chalamila ametoa pole kwa Serikali kufuatia maafa yaliyotokea huko Katesh wilayani Hanang' Mkoa wa Manyara kutokana na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha Desemba 3, mwaka huu

"In facts Tanzania is a big country, specific mkutano huu unafanyikia katika Mkoa wa Dar es Salaam ambao sisi ndiyo host wenu.

"Na kwa mamntiki hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu kabla siajeleza mambo mengi nikupe pole sana wewe pamoja na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kile kilichotokea kule Hanang' ambacho kimesababishwa na mafuriko na tope ambapo watu wamepoteza maisha na wengine ambao wamepata madhara pamoja na kubomoka kwa miundombinu kule Hanang'.

"Kwa hiyo, tunakupa pole sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu tumeona jitihada kubwa ambazo umekuwa ukizifanya."

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Chalamila amemweleza Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwa Mkoa wa Dar es Salaam hakuna mafuriko.

"Mheshimiwa Waziri Mkuu, hapa kwetu Dar es Salaam siku chache zilizopita tumebadilisha tafsri ya neno mafuriko kama ambavyo ilikuwa imezoeleka zamani, ilikuwa kila maji yanapotuwama mahali wanaita mafuriko.

"Lakini, tumepitia tukagundua ni maji yanayokwamishwa na watu kwa kuziba njia za maji kuelekea mahali pake, kwa hiyo mpaka muda huu bado hatuja-experience mafuriko pamoja na mvua nyingi ambazo zinaendelea kunyesha katika mkoa wetu wa Dar es Salaam,"amefafanua Mheshimiwa Chalamila.

Naye Katibu Mkuu wa AfCFTA, Wamkele Mene amesema, mafanikio yamepatikana katika Maendeleo ya Itifaki ya Wanawake, Vijana na Biashara ambapo mawaziri wa biashara watajadiliana kufikia makubaliano ambayo yatawasilishwa Februari 2024 katika Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali ili ithibitishwe

Mene amebainisha kuwa, takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya biashara zote barani Afrika ni biashara ndogo na za kati (SMEs).
 
Aidha,asilimia 60 zinamilikiwa na wanawake, ambapo zinachangia asilimia 80 ya uzalishaji wa ajira na kuchangia asilimia 40 ya Pato la Taifa la Afrika kwa pamoja.

Vilevile amesisitiza kuwa, ni muhimu kujua kwamba Itifaki ya Wanawake na Vijana katika nafasi za biashara inaweka Bara la Afrika kwa wanawake katika biashara kunufaika kupitia maendeleo ya kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news