Rhobi Samwelly aendelea kuwa daraja la kiuchumi kwa wanawake mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

WANAWAKE wajasiriamali Tarafa ya Nyancha Wilaya ya Rorya mkoani Mara wamemshukuru Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly kwa kuwaunganisha na na fursa za mikopo ya bila riba ambayo wataanza kunufaika nayo itakayotolewa na Benki ya CRDB kupitia taasisi yake ya CRDB Foundation zao la EMBEJU katika vikundi vyao ili kuinua biashara zao waweze kuwa na uchumi imara.
Wakizungumza leo Desemba 21, 2023 wakati wa mafunzo ya ujasiriamali ambayo yameendeshwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kupitia Programu ya Erasto Widows Empowerment Programme wamesema, matarajio yao ni kuona wakiinuka kiuchumi kwa kuendeleza biashara zao.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na wanawake wajasiriamali zaidi zaidi ya 1,000 ambapo pamoja na mambo mengine wamepata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali ya kibiashara na kupatiwa majibu kutoka kwa maafisa wa Benki ya CRDB ambao pia wameendesha zoezi la ufunguaji wa akaunti kwa wajasiriamali hao.

Jesca Anyari mkazi wa Shirati amesema kuwa, Rhobi amewatia hamasa wanawake wajasiriamali kuunda vikundi vya watu 30 na kuwaunganisha na CRDB ambapo wamenufaika na elimu ya ujasiriamali kwanza na pia watapata mikopo isiyo na riba katika kuhakikisha wanakuza biashara zao na ili wawe na uchumi thabiti.

Veronica Omondi amesema kuwa, baadhi ya wajasiriamali wamekuwa walishindwa kukuza biashara zao kutokana na kukosa mitaji, lakini kupitia vikundi ambavyo wameviunda na kuhakikisha kupata mikopo kwake ni neema kubwa malengo yake ni kukuza biashara yake ya nguo anayoifanya na faida atakayopata imsaidie kusomeshwa watoto wake na kuhudumia familia,kwani ni mjane.

"Nimpongeze Rhobi, amekuwa na mwendelezo mzuri wa kututia hamasa wanawake tusibweteke bali tuchakarike.

"Hili ni jambo zuri sana, alituhamasisha tuunde vikundi na sisi tukaunda akasema atashirikisha watu wa CRDB wanatoa mikopo bila riba ila ina ada ndogo na bima," amesema Grace Okoth na kuongeza.

"Binafsi nilipokea kwa furaha kwani nina biashara yangu ya matunda, tumekuwa tukilipa kwa watu binafsi kwa riba kubwa, lakini hii fursa ni nzuri sana, nikasema nijiunge kwenye kikundi nikipata mkopo nitapanua biashara yangu.

"Baadhi yetu kinamama walikuwa wakiogopa, lakini alitupa hamasa na kutuambia tuwe na uthubutu na kweli tumeitikia kwa wingi sana," amesema Grace Olamu.

Verediana Fabian amesema,"wanawake tunahitaji kuungwa mkono na kupewa hamasa wapo wanawake ambao wamekuwa wakiogopa kukopa, na wengine kukopa mikopo ya riba kubwa na masharti mengi maarufu kausha damu.

"Lakini tunapokuwa na wanawake ambao wana ujasiri kama Rhobi kutupa hamasa, elimu na kutujenga kisaikolojia tutafika mbali kiuchumi na kuona fursa zinazotuzunguka na kuweza kuzitumia kwa faida,"amesema.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly akizungumza na wanawake hao amesema kuwa wanawake wakiwa na uchumi imara maendeleo katika familia yatapatikana na kupunguza vitendo vya ukatili wa Kijinsia.

Amesema, wataendesha biashara zao na kujipatia kipato ambacho pia kitachangia kusomesha watoto wao, kuhudumia familia na kushirikiana na waume zao kupanga na kufanya maendeleo ya familia, huku akisema atasimama pamoja na wanawake mkoani Mara na taifa kwa ujumla kuona wanawake wanapiga hatua katika maendeleo na kuondokana na vitendo vya ukatili wa Kijinsia vinawavyokandamiza.

Killian Anthony Manyoni ni Meneja wa Benki ya CRDB Matawi ya Shirati na Rorya amesema, kuwa Benki ya CRDB katika kuwasaidia wanawake imeanzisha taasisi nyingine ya kuwasaidia wanawake na vijana ambayo iko nje na mfumo wa kibenki ijulikanayo kwa jina la IMBEJU.

Amesema,ipo kwa ajili ya kuona wanawake wajasiriamali wanapiga hatua kwa kuinua biashara zao kwa kuwakopesha bila riba.

Amesema,mkopo huo una ada ya asilimia sita na malipo ya bima asilimia moja na ni tofauti na mikopo mingine ya kawaida ambayo hutolewa, kwani huwa ina riba na masharti ambayo si rahisi kwa baadhi ya wajasiriamali wadogo kuyamudu, lakini kupitia EMBEJU katika vikundi vyao wataneemeka.
Ameongeza kuwa, mkopaji atarudisha mkopo wake ndani ya miezi mitatu hadi miezi 12 na atakuwa ndani ya kikundi huku akisema ni mkopo ambao shabaha yake ni kumwinua Mwanamke Mjasiriamali akue kiuchumi na achangie katika maendeleo ya familia yake na taifa pia.

Amesema,mdhamini atakuwa ni kikundi ambacho Mjasiriamali huyo atakuwa amejiunga. Na mkopo utarudishwa kwa kila wiki na kila mwezi kutegemeana na uendeshaji wa biashara na aina ya biashara ambayo mkopaji anaifanya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news