Serikali yatoa msisitizo kwa Bodi ya Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana

ZANZIBAR-Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi, na Utawala Bora, Mhe. Haroun Ali Suleiman amewataka watendaji wa bodi ya uongozi wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana kufanya kazi kwa mashirikiano ili kuleta mabadiliko ya kiutendaji katika bodi hiyo.

Akitoa nasaha kwa wajumbe wa bodi ya sita ya uongozi wa kamisheni ya wakfu na mali ya amana wakati akiizindua bodi hiyo huko Ukumbi wa Katiba na Sheria Mazizini Zanzibar Mwalim Haroun amesema lengo la uwepo wa bodi hiyo ni kudhibiti na kusimamia mali za wakfu kwa maslahi ya Nchi na jamii ya waislamu.

Amesema, matarajio yake katika bodi hiyo ni kuona mali zinazotolewa za wakfu zinaendelea kuwanufaisha walengwa,watoaji na taifa kwa ujumla na kuwataka kuzifanyia uwekezaji mali hizo ili ziweze kuzalisha na kuisaidia jamii ya kiislamu katika kujiendeleza kiuchumi na kutaraji malipo kutoka kwa allah.

Aidha, aliwataka wajumbe hao kufanya kazi kwa imani, huruma na kwa kufuata miongozo na sheria ili kuhakikisha maslahi ya waislamu yanapatikana sambamba na kusimamia na kuyatekeleza vyema yale yote yalioachwa na bodi iliyomaliza muda wake.

Awali alitangulia kusema kuwa wizara imeridhishwa na utendaji kazi wa bodi iliyopita na serikali kuendelea kutambua mchango wa taasisi hiyo pamoja na kuitaka bodi mpya kuendeleza pale ilipofikia bodi iliyomaliza muda wake ili kuhakikisha malengo waliyojiwekea yanafikiwa.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe waliomaliza muda Mwenyekiti wa bodi ya tano ya uongozi wa kamisheni ya wakfu na mali ya amana, Prof. Hamed Rashid Hikmany amesema kamisheni hiyo ni taasisi kubwa inayotegemewa na jamii ya waislamu hivyo waliishauri bodi mpya kutekeleza mapendekezo ya mageuzi ya kiutendaji na uwajibikaji katika sekta hiyo yaliyotolewa na bodi iliyomaliza muda wake .

Walifahamisha kuwa taasisi hiyo ni tasisi inayoshugulika na fedha za jamii ya waislamu ikiwemo mirathi,wakfu, zaka na hija hivyo waliwashauri kuzitunza vyema kwa maslahi ya waliozitoa ,walengwa na jamii kwa ujumla pamoja na kuanzisha uwekezaji ili kuzizalisha mali hizo na kuendelea kutumika siku hadi siku na kuleta tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, waliiasa jamii kuacha tabia ya kuchukua majengo na ardhi zilizotolewa kwa ajili ya allah na kuwataka wale wote waliochukua mali hizo kuzirudisha kwani mali hizo zimetolewa kwaajili ajili ya Allah.

Mwenyekiti wa bodi mpya ya wakfu na mali ya amana, Prof.Issa Haji Zidi amesema, wajumbe wamepokea uteuzi huo na kuahidi kufanyakazi kama vile uislamu unavyoelekeza juu ya kusimamia majukumu ya wakfu na mali amana pamoja na kutekeleza vyema mikakati yote iliyowekwa na bodi iliyopita ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Alisema, bodi hiyo itafanya kazi zake kwa ushirikiano na kuahidi kuitoa kamisheni hiyo katika sehemu moja na kwenda sehemu nyengine kimaendeleo ili kukidhi matakwa ya Rais kupitia wizara ya katiba na sheria na kuomba watendaji wa wizara,jamii na serikali kuwapa ushirikiano katika kukamilisha majuku yao.

Nao baadhi ya wajumbe wa bodi hiyo akiwemo Shekh Suwedi Ali Suwed na Balozi Mohammed Haji Hamza wamesema taasisi hiyo ni muhimu katika nchi na dini ya kiislamu na kuahidi kuwa bodi hiyo itaisaidia serikali katika kuhakikisha masuala ya wakfu , zaka hija na sadaka zinawafikia walengwa.

Aidha, Balozi Mohammed alisema ataimarisha mashirikiano na mahusiano ya kitaifa na kikanda kwa maslahi ya kamisheni, waislam na Zanzibar kwa ujumla.
Kamisheni ya wakfu na mali ya amana Zanzibar ilizindua bodi ya sita ya uongozi mara baada ya kumalizika kwa muda wa bodi ya tano ya kamisheni hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news