Ajali zitapungua

NA LWAGA MWAMBANDE

KWA mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa Desemba, 2023 huko Geneva nchini Uswisi ilibainisha kuwa, ingawa vifo vya kila mwaka vimepungua kwa asilimia tano na kufikia takribani milioni 1.2, bado ajali za barabarani zimesalia kuongoza kwa kusababisha vifo vya watoto na vijana kuanzia umri wa miaka mitano hadi miaka 29 duniani.

Ripoti hiyo Hali ya Usalama Barabarani mwaka 2023 (Global Status Report on Road Safety 2023) ni ya kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi 2021, na ni ya tano kutolewa na WHO tangu ianze kufuatilia masuala ya ajali barabarani na kuweka mipango ya kuchukua hatua.

WHO inafafanua kuwa, ajali za barabarani zinaongeza shinikizo kwenye mifumo ya afya duniani ambapo waenda kwa miguu, waendesha baiskeli na watumiaji wengine wa barabara walio hatarini, wanakabiliwa na hatari ya kuathirika afya zao.

Dkt. Tedros Ghebreyesus ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa WHO alifafanua kuwa,idadi ya vifo vitokanavyo na ajali barabarani inaelekea kwenye mwelekeo mzuri, kwani inapungua.

"Ajali za barabarani zinazuilika. Tunatoa wito kwa nchi zote kutoa kipaumbele kwa watu na sio magari pindi zinapopanga miundombinu yao ya usafirishaji, na zihakikishe usalama wa waenda kwa miguu, waendesha baiskeli na watu wengi walio katika mazingira magumu.”

Hata hivyo, miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa nchi 108 ziliripoti kupungua kwa vifo vitokanvyo na ajali kati ya mwaka 2010 na 2021.

Nchi 10 zimefanikiwa kupunguza vifo kwa asilimia 50. Nchi hizo ni Belarus, Brunei Darussalam, Denmark, Japan, Lithuania, Norway, Uruai, Trinidad na Tobago, Falme za Kiarabu na Venezuela.
Vile vile, nchi 35 nyingine zimepiga hatua kupunguza vifo vitokanavyo na ajali kwa kati ya asilimia 30 na 50.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunapokuwa barabarani tunazifuata sheria za usalama barabarani, kwani ni tiba moja wapo ya kukomesha ajali. Endelea;

1.Ni wajibu wetu sote, tuwapo barabarani,
Kufwata sheria zote, zile za barabarani,
Ni kwa madereva wote, walioko safarini,
Tukizifwata sheria, ajali zitapungua.

2.Matukio mengi sana, ajali barabarani,
Uzembe ni mwingi sana, tuwapo barabarani,
Kwetu ni hasara sana, twawahishwa mautini,
Tukizifwata sheria, ajali zitapungua.

3.Kwanza huu mwendo kasi, tuwapo barabarani,
Matokeo yake hasi, kwa wengi barabarani,
Tasingizia mkosi, tukifika msibani,
Tukizifwata sheria, ajali zitapungua.

4.Kuna alama za mwendo, zinaonyesha njiani,
Dereva waweka kando, wakimbia marathoni,
Hujui huo ni mwendo, kuelekea kifoni?
Tukizifwata sheria, ajali zitapungua.

5.Watafiti wanasema, hata mimi naamini,
Upande wa kinamama, madereva ni makini,
Alama wanazisoma, wazingatia njiani,
Tukizifwata sheria, ajali zitapungua.

6.Fanyia matengenezo, ndipo nenda safarini.
Gari imara ni nguzo, kutokukwama njiani,
Kukwama hovyo tatizo, ajali barabarani,
Tukizifwata sheria, ajali zitapungua.

7.Simu twazipenda sana, zatutia hatarini,
Huko tunazama sana, tuwapo barabarani,
Tunajisahau sana, twajikuta ajalini,
Tukizifwata sheria, ajali zitapungua.

8.Tuache tabia hii, kutega tega njiani,
Tukijua mara hii, wajeda hatuwaoni,
Twakanyaga nanihii, bila ya hofu njiani,
Tukizifwata sheria, ajali zitapungua.

9.Wito ninautoa, wakuu barabarani,
Alama mnazotoa, zinatufaa njiani,
Zile walizobomoa, turudishie jamani,
Tukizifwata sheria, ajali zitapungua.

10.Mstari katikati, kugawa barabarani,
Huo ni muhimu ati, hasa usiku njiani,
Huo mwema mkakati, kutoondoka reline,
Tukizifwata sheria, ajali zitapungua.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news