Askofu Malasusa:Mtumikie Yehova

NA LWAGA MWAMBANDE

LEO Januari 21,2024 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameshiriki ibada ya kuingizwa rasmi kazini Baba Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Katika ibada hiyo, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amempa ujumbe Baba Askofu huyo kuwa, "Mwenyezi Mungu aliyekuita, na wewe kuitika kwa kazi hii ya kutumikia watu wake akakusimamie na kukuongoza. (Tafakari: Mithali 3:5-6).

"Nakuahidi ushirikiano wangu na Serikali katika utekelezaji wa jukumu hili, ikiwa ni pamoja na kazi ya kuendelea kuimarisha uchumi wetu, demokrasia yetu, utoaji haki, umoja na mshikamano wetu, na kuendelea kutunza amani ya nchi yetu.

"Ili wananchi waendelee na shughuli zao mbalimbali za ujenzi wa Taifa lao na ustawi wao, ikiwemo kutekeleza haki yao ya kuabudu,"amebainisha Rais Dkt.Samia.

Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande yeye anaendelea kusisitiza kuwa,Baba Askofu Dkt.Malasusa aendelee kumtumikia Mungu. Endelea;

1.Alishakuwa mkuu, karejeshewa ukuu,
Ni utumishi mkuu, kwake Mungu alojuu,
Nafasi hii ya juu, heshima kwa Mungu juu,
Askofu Malasusa, mtumikie Yehova.

2.Mungu kajichagulia, kiongozi kuwa juu,
Kanisa kuangalia, lifanye ya Mungu juu,
Heri tunamtakia, baraka za Mungu juu,
Askofu Malasusa, mtumikie Yehova.

3.Neno la Mungu lasema, kwa mtu aliye juu,
Nafasi ya kusimama, chini Mungu awe juu,
Unyenyekevu twasema, kwake Mungu ni ukuu,
Askofu Malasusa, mtumikie Yehova.

4.Japo kura zinapigwa, mwamuzi ni Mungu juu,
Hapo mwovu anazugwa, askofu kazi kuu,
Yote maovu hubwagwa, Mungu anabaki juu,
Askofu Malasusa, mtumikie Yehova.

5.Askofu Malasusa, sasa nchini mkuu,
Ni kwa Walutheri hasa, kanisa lililo juu,
Injili washika hasa, ya Mungu aliye juu,
Askofu Malasusa, mtumikie Yehova.

6.Kanisa kwake imani, ni kwa Mungu alo juu,
Neno linalithamini, mafundisho liko juu,
Semina maombi dini, tumjue Mungu juu,
Askofu Malasusa, mtumikie Yehova.

7.Ni nani asiyejua, Walutheri wako juu,
Jamii inawajua, kwa huduma zilojuu,
Sipitali twazijua, shule na vyuo vikuu,
Askofu Malasusa, mtumikie Yehova.

8.Tunamuomba Rabuka, Mungu wetu alo juu,
Ili aweze mshika, huyu aliye mkuu,
Hatamu aweze shika, apendavyo Mungu juu,
Askofu Malasusa, mtumikie Yehova.

9.Ni mengi matumaini, kwetu na kwa Mungu juu,
Kuvipata vya rohoni, kutoka kwake mkuu,
Ili idumu imani, kwake Mungu alo juu,
Askofu Malasusa, mtumikie Yehova.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news