DCEA yamdaka Mtanzania kinara wa dawa za kulevya duniani

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imemkamata kinara wa mtandao wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya aina ya Cocaine ndani na nje ya nchi.
Sambamba na kukamata jumla ya gramu 692.336 za Cocaine zinazowahusisha watuhumiwa wanne katika operesheni maalumu zinazoendelea nchini.

"Huyu mfanyabiashara ni mkubwa kwa wiki ana uwezo wa kusafirisha watu 10 (punda) kwa ajili ya kupeleka dawa za kulevya maeneo mbalimbali duniani, kibaya zaidi anatumia watoto wa maskini kuwabebesha dawa za kulevya na wengi wanafia njiani;

Hayo yameelezwa leo Januari 24,2024 katika ofisi za mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali, Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema, kinara huyo ambaye alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu alikamatwa maeneo ya Boko Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

"Mfanyabiashara huyo wa mtandao wa Cocaine ambaye alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu alikamatwa katika eneo la Boko Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam pamoja na washirika wake watatu.

"Ambapo kati yao wawili walikamatwa jijini Dar es Salaam na mmoja alikamatwa katika Kijiji cha Shamwengo Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya,"amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa, dawa ya kulevya aina ya Cocaine ambayo huzalishwa kwa wingi katika Bara la Amerika Kusini husafirishwa kwa njia ya anga na wabebaji (punda).

Amesema, huwa wanazimeza zikiwa katika mfumo wa pipi ambapo kwa mara moja mtu hubeba kuanzia gramu 300 hadi 1,200 na wengine hadi gramu 2,000 kwa wakati mmoja.

"Mfanyabiashara aliyekamatwa ana mtandao mkubwa wa wabebaji (punda) kutoka nchi mbalimbali ambao huwatumia kusadawa hizo kwa njia ya kumeza.

"Hivyo, makosa yake yanaangukia katika uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka,"amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Vile vile, DCEA imetangaza operesheni kali ya dawa za kulevya 2024 ambayo itafanyika nchi kavu na baharini.

Amesema, operesheni hizo nchi kavu zitahusisha mashamba ya dawa za kulevya, kwenye mipaka, maeneo ya mijini kwenye vijiwe vya usambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya.

Kwa upande wa baharini, operesheni zitahusisha fukwe na katikati ya bahari. Pia, amesema operesheni hizo zitahusisha maeneo yote yanayouza shisha ili kubaini matumizi ya dawa za kulevya.

"Operesheni hii itahusisha pia maeneo yote wanayouza shisha ili kubaini matumizi ya dawa za kulevya ambapowale wotè watakaòbainika kutumia dawa hizo kupitia shisha watachukuliwa hatua kali za kisheria.

"Vilevile operesheni hii itahusisha wauzaji wanaokiuka taratibu za uuzaji wa dawa tiba zenye asili ya kulevya na kemikali bashirifu,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Pia, ametoa onyo kwa wote watakaoendelea kujihusisha na uzalishaji, biashara na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini kuacha, kwani serikali imeendelea kuiwezesha mamlaka hiyo kwa kununua vifaa vya kisasa na mafunzo kwa watumishi ili kuwajengea ujasiri na weledi katika kutekeleza operesheni kwa ufanisi mkubwa.

“Hivyo kwa wale wote watakaoendelea na kilimo cha bangi, mirungi na biashara ya dawa za kulevya za viwandani watashughulikiwa ipasavyo.

“Mamlaka inawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za watu wote wanaojihusisha na biashara za dawa za kulevya ili kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa salama kwa kupiga simu namba ya bure 119 na taarifa zitapokelewakwa kwa usiri mkubwa na kufanyiwa kazi,”amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news