Mziha kuanza kutoa huduma za Afya

MOROGORO-Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume ameagiza Kituo cha Afya Mziha kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro kuanza kutoa huduma Januari 29, 2024 kutokana na ujenzi wake kukamilika.
Akizungumza Januari 27, 2024 kwenye ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Mvomero na Kituo cha Afya Mziha mkoani Morogoro, Dkt.Mfaume amesema majengo yote yamekamilika likiwamo jengo la OPD, maabara, jengo la upasuaji, jengo la mama na mtoto na kichomea taka na baadhi ya vifaa na vifaatiba vipo na watumishi wapo.

"Watumishi wa afya hakikisheni mnafanya kazi na kutimiza majukumu yenu ya kuwahudumia wananchi, majengo haya yaendana na utoaji wa huduma bora kwa wananchi muwahudumie kwa lugha nzuri," amesema.

Aidha,Dkt. Mfaume amekemea tabia zinazofanywa na baadhi ya watumishi ambazo sio nzuri akieleza Serikali inajenga nyumba za watumishi karibu na hospitali ili kurahisisha utoaji wa huduma lakini inapotea dharura ya mgonjwa mtumishi anapohitajika kutoa huduma wakati mwingine hutoa lugha sio nzuri na hukataa kutoa huduma.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mziha Mhe.Adam Haule na mkazi wa eneo hilo, Anna Chengula wameishukuru Serikali kwa Kuwajengea kituo hicho ambacho kitapunguza vifo vya mama na mtoto kwa kuwa kabla ya kituo hicho wajawazito walilazimika kutembea takribani kilomita 60 kufuata huduma za afya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news