Raphael Maganga ndiye CEO mpya TPSF

NA GODFREY NNKO

BODI ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imemteua, Bw. Raphael Maganga kuwa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) mpya.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti, Bi.Angelina Ngalula kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya TPSF.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi wa Raphael Maganga unaanza Februari Mosi,2024.

Maganga anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Afisa Mtendaji Mkuu, John Ulanga.

Septemba 26,2023 John Ulanga aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Tangu wakati huo hadi leo majukumu yake yaliendelea kutekelezwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Raphael Maganga.

Imeelezwa kuwa, Bw. Maganga analeta uzoefu na utaalamu mwingi katika maendeleo ya sekta binafsi, diplomasia ya uchumi na uwekezaji na biashara akiwa amefanya kazi nchi kadhaa kama vile China,Australia na Kenya.

Kabla ya kujiunga na TPSF mwaka 2021 kama mshauri wa sekta binafsi, aliwahi kuwa mwakilishi wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) kwa Tanzania na Burundi shirika lililolenga kushughulikia mazingira ya biashara katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Bw.Maganga alianzia kazi katika benki ya AMP Capital kama Mshauri wa Fedha na Uwekezaji kabla ya kuhamia Domain Wealth Services chini ya Westpac Bank moja ya Benki kubwa nchini Australia.

Pia,amefanya kazi kama mshauri wa uwekezaji katika ofisi binafsi ya Makamu wa Rais mstaafu nchini Kenya mwaka 2015-16 kabla ya kurejea Tanzania na kuwa Mtendaji Mkuu wa Rakestar Group na baada ya hapo kwenda kwenye Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC).

Bw. Maganga, ana Shahada ya Biashara (Uhasibu na Fedha) kutoka Chuo Kikuu cha Monash nchini Australia na Stashahada ya Uzamili ya Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Kituo cha Mahusiano ya Kigeni, na Wahitimu wa CAPSTONE 13 kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi.

"Bodi ya Wakurugenzi ina imani kamili na maono na uongozi wa Bw. Maganga katika kuhakikisha sekta binafsi nchini Tanzania inaendelea kuwa shindani. Bodi inamtakia mafanikio katika majukumu yake mapya;

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news