RC wa Tabora aipongeza Maliasili na Utalii kwa jitihada za kukuza utalii mkoani humo

NA BEATUS MAGANJA

MKUU wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Batilda Salha Burian ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA kwa jitihada za dhati za kukuza utalii Mkoani Tabora.
Dkt. Batilda alitoa pongezi hizo Januari 15, 2024 alipotembelewa na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda ofisi kwake akiwa katika ziara ya kikazi Kanda ya Magharibi iliyokuwa na lengo la kukagua shughuli za uhifadhi na utalii zinazofanywa na TAWA Mkoani humo.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema anatambua jitihada zinazofanywa na TAWA katika kuboresha miundombinu ya utalii katika bustani ya Wanyamapori Mkoani humo ijulikanayo kama Tabora ZOO na kuishauri Mamlaka hiyo kuangalia uwezekano kuongeza miundombinu katika bustani hiyo kwa ajili ya kuongeza mapato.

Vilevile, alishauri kuongeza mazao mbalimbali ya wanyamapori kama vile sumu ya nyoka ambapo alisema kuwa inahitaji utafiti zaidi.
Pia Dkt. Batilda alisema ili kuendelea kuchagiza shughuli za utalii Mkoani humo, TAWA ione namna bora ya kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali yenye vivutio vya utalii ikiwemo bustani ya wanyamapori ya Tabora.

Aidha, aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa TAWA ili kuhakikisha shughuli za Uhifadhi na Utalii zinazofanywa na taasisi hiyo zinazidi kuimarika.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda alimshukuru Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora kwa ushirikiano na mshikamano anaoutoa kwa taasisi yake anayoiongoza katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kiuhifadhi na utalii mkoani humo.
Ziara ya Kamishna Mabula katika Kanda ya Ziwa, Kati na Magharibi ililenga kukagua shughuli mbalimbali za uhifadhi na utalii zinazofanywa na TAWA katika Kanda hizo ikiwa ni pamoja na kukagua miradi mbalimbali kama vile ujenzi wa karakana ya kutengenezea magari na mitambo wilayani Manyoni.

Pia kuzindua jengo la ofisi ya Pori la Akiba Moyowosi Wilayani Kibondo na kutembelea familia za ndugu walioathiriwa na wanyamapori aina ya mamba na kuwapa pole katika vijiji vya Kasahunga na Mayolo wilayani Bunda

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news