TARURA yarejesha mawasiliano Dar

DAR ESSALAAM-Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) imefanikiwa kurejesha mawasiliano ya miundombinu katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam na hivyo wananchi kuendelea na shughuli zao kiuchumi na kijamii.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga wakati wa ukaguzi wa miundombinu katika Wilaya ya Kinondoni, Temeke na Ubungo.

Mhandisi Mkinga amesema kwamba TARURA imejipanga kukabiliana na uharibifu uliojitokeza na kutekeleza agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha mawasiliano yanarejeshwa na kwamba hakuna shughuli zitakazokwama na kuongezeka kwa gharama za usafiri kutokana na kukosekana kwa mawasiliano.

“Sisi kama TARURA toka tarehe 21 Januari,2024 tumefanya kazi kwa 'speed' usiku na mchana na tutaendelea kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii zinarejea kama awali kwa wakazi wote wa mkoa huu.”
Amesema,mvua nyingi zilizonyesha hivi karibuni zilileta madhara makubwa kwa sababu ya ardhi kujaa maji na kupelekea barabara nyingi kuathirikia hususan madaraja.

“Mvua zilizonyesha tarehe 20 na 21 Januari, 2024 zilileta madhara makubwa ambapo kingo za madaraja ziliathiriwa na maji.

“Madaraja mengi yamebaki mazima lakini maingilio ya daraja ambayo sehemu ya tuta lake zimesombwa na maji, udongo ulijaa maji hivyo ilikuwa rahisi kuondoka kila maji yalipokuwa yamezidi kwenye madaraja yetu mengi.”

Mhandisi Mkinga alitaja madaraja yaliyoathiriwa ni pamoja na daraja la Ally Hushumu, Mbopo, Madale, Msumi, Tanganyika, Majengo, Bwege pamoja na daraja la Msumi (Kivule).
Aliongeza Madaraja yaliyoathirika kabisa na hivyo tunahitaji kuyajenga upya hadi hali ya hewa itakapotulia ni daraja la Msumi-Kivule (Ilala) ambalo limewekwa kivuko cha watembea kwa miguu pamoja na daraja la Msumi (Madale - Kinondoni) ambalo watatengeneza kivuko cha watembea kwa miguu kwani daraja hilo limeharibika zaidi na haliwezi kutengenezwa kwa haraka.

Aidha,Mhandisi Mkinga alieleza kuwa tayari ujenzi mpya wa daraja hilo pamoja na Barabara ya Mbezi Msumi – Madale Km 8.5 utafanyika chini ya Mradi wa DMDP 2 ambao unatarajia kuanza Mei, 2024.
Kuhusu Daraja la Ally Hushumu amesema, maingilio yote yametengenezwa hivyo linapitika kwa sasa.

"Kama mnavyoona huku kuna wanafunzi zaidi ya 250 wanasoma upande mwingine hiyo ndio njia yao ya kwenda shule na pia kuna watumiaji wengine katika shughuli zao za kijamii,"amesema.
Barabara ya Madale – Bunju ambayo ilikatika sehemu mbili, Mabanda ya Kuku Km. 8 kutoka Madale na daraja la Mbopo Km. 2 kutoka Madale na hivyo wananchi wote ndani ya Km. 6 hawakuwa na njia mbadala ya kutumia na hadi Ijumaa wamesharejeshewa mawasiliano.

“Daraja la Tanganyika lilipo Salasala – Benako ambalo maingilio yake yalikuwa yamekatika nalo tumesharejesha mawasiliano na sasa tunaendelea kujaza tuta ili maji yakija tena yasilete madhara.”

Hata hivyo amesema, wamesharejesha barabara ya Salasala-Benako,Goba-Majengo-Kinzudi na kuimarisha maingilio ya daraja la kwa Bwege na njia za kuingilia barabara hizo zimeshakamilika.
Kwa upande wa Temeke jumla ya barabara 15 zenye urefu wa Km. 15.02 na madaraja mawili ziliathirika kwa kiwango kikubwa na wameweza kurejesha mawasiliano barabara ya Toangoma-Sokoni.

Kigamboni barabara ya Mivumoni iliathiriwa sana hivyo wamepanga mawe na sasa inatumika ila wameshampata mkandarasi ambaye atatengeneza barabara hiyo kwa kunyanyua tuta na kuweka vizuizi vya kuchepusha maji ili iweze kupitika muda wote.

”Barabara ya Dege-Mbutu nayo inasubiri mvua ikatike ili itengenezwe na iweze kupitika."

Pia upande wa Ilala-Ukonga, Mhandisi huyo amesema wameshafanyia tathmini barabara za upande huo na sasa wanajipanga kwenda kufanyia matengenezo barabara ya Banana – Kitunda – Msongola na Kivule Hospitalini ambazo zipo kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami kupitia (DMDP-2) na tatizo la kukosekana mifereji litaenda kutatuliwa.
Kwa Barabara za Ulongoni – Pepeteka – Mwembesupu – Mwembekiboko - Bangulo km 2.5, Banana – Kitunda – Kivule – Msongola km 9.28, Kitunda - Magore 2.89Km, Kitunda – Mwanagati – Kwa Mpalange km 6.5, Mombasa - Kivule km 6.84, Mkolemba – Kivule - Mzunguuko km 1.93, Kwa Diwani - Bombambili km 6.14, Gongolamboto – KIU –Radar - Majohe 4.35Km, Nguvu Kazi - Yongwe km 6.0, Pugu – Majohe – Mbondole – Njia Nne km 12.2 .

“Hizi zilizopo Jimbo la Ukonga nazo zimeathirika na mvua,zimekwishafanyiwa tathimini ya maboresho ya kawaida na tunasubiri mvua ipungue tuweze kuanza kazi ya kurejesha hali ya awali.”

Hata hivyo amesema kutokana na tathmini ya kuangalia maeneo ya Jiji yaliyoathiriwa na mvua Serikali itakuja na mpango wa kujenga mifereji ya mvua na kuondosha hali ya mafuriko na kuzagaa kwa maji katika makazi ya watu kila mara mvua zinaponyesha kwa hali hiyo tatizo hilo itaenda kuondoka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news