Theluthi mbili ya nchi duniani zakusanyika jijini Kampala

KAMPALA-Takribani theluthi mbili ya nchi duniani zimekusanyika jijini Kampala, Uganda kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) wenye nchi Wanachama 120 na Mkutano wa nchi za Kundi la 77 na China (G77+China) lenye Wanachama 134.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama hai wa jumuiya hizo, hivyo inashiriki kikamilifu katika ngapi zote za Mikutano hiyo iliyoanza tarehe 15 Januari na itahitimishwa tarehe 22 Januari 2024.

Kwa ngazi ya Mawaziri, Mhe. January Makamba (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa siku mbili wa ngazi ya Mawaziri uliokamilika jana tarehe 18 Januari 2024.

Pembezoni mwa Mkutano huo, Mhe. Makamba alifanya jitihada kubwa za.kukutana na Mawaziri wenzake kwa lengo sio tu la kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na nchi marafiki, bali pia kuweka mikakati ya kushirikiana kiuchumi.
Mhe. Makamba hadi tarehe 18 Januari 2024 alikutana na Mawaziri saba wa Mambo ya Nje kutoka Kenya, Mhe. Dkt. Musalia Mudavadi; Somalia, Mhe. Ali Mohammed Omar; Ghana, Mhe.Shirley Ayorkor Botchwey; Ethiopia, Mhe. Demeke Mekonnen; DRC, Mhe. Christophe Lutundula; Venezuela, Mhe. Yván Gil Pinto na Bahamas, Mhe. Alfred Seers.
Mhe. Waziri anaendelea kukutana na Mawaziri wenzake na agenda kubwa ni mikakati ya kuhakikisha kuwa Tanzania na nchi marafiki zina nufaika kwa kuweka mazingira rafiki ya Biashara, uwekezaji na kuondoa changamoto zinazokwamisha jitihada za kukuza Uchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news