Ushirikiano wetu katika kusimamia mali za umma hauepukiki-Mchechu

ZANZIBAR-Ofisi ya Msajili wa Hazina Tanzania Bara imesema, ushirikiano kati ya ofisi hiyo na Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar ni njia moja wapo ya kuleta mabadiliko ya kukuza uchumi kwa ustawi bora wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Msajili wa Hazina Tanzania Bara, Nehemiah Mchechu huko katika Ofisi ya Msajili wa Hazina Maisara jijini Zanzibar. 

Msajili huyo alifanya ziara katika ofisi hiyo kwa lengo la kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili za umma.

Mchechu akizungumza na waandishi wa habari amebainisha kuwa, wanakwenda kubadili sheria ili waendane na kasi ya uchumi anayoitaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Amesema, Serikali ipo katika mkakati wa kukuza na kukuimarisha uchumi wa nchi, kwani ukuaji wa uchumi unaenda kwa kasi hivyo ni vyema kuwa makini katika kusimamia na kuweka mpango mkakati ili kufikia malengo.

Mchechu amesema kuwa, lengo la ziara hiyo ni kubadilishana uzoefu na kupeana ujuzi wa kiutendaji katika kazi zao za kila siku ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano waliyotiliana saini Aprili,2023 ili kuleta ufanisi.
“Ushirikiano kati yetu katika utendaji wa kazi zetu ni jambo lisiloepukika kwa vile sote tunafanya kazi moja ya kusimamia mali za umma,”amefafanua Mchechu.

Ameongeza kuwa, ni wajibu wao kuhakikisha taasisi zote za Serikali zinafanya vizuri katika kusimamia mali za umma na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria endapo taasisi hizo zitakwenda kinyume na shrria za usimamizi wa mali za umma.

Katika hatua nyingine,Mchechu ameeleza kuwa, katika kuimarisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wasajili wamekubaliana kuongeza weledi katika kusimamia mashirika kwa manufaa ya umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliongeza kuwa, pia wameamua kubadilishana wafanyakazi na uzoefu wa watendaji kitaalamu pamoja na kuwa kioo cha ufanisi wa utendaji kazi kwa kushiriki kikamilifu katika kudumisha Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Kuhusu TR

Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya Umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya Sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa Ofisi inayojitegemea kimuundo.

Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) Ofisi ilikabidhiwa majukumu ya shirika hilo.

Naye Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Muhammad Sanya ameeleza kuwa, Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar kwa sasa inasimamia mashirika 17 na imejipanga kuhakikisha mashirika hayo yanaleta tija kulingana na malengo ya kukuza uchumi kutokana na maono ya Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi.

Zanzibar

Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar imeanzishwa kwa Sheria Nambari. 6 ya mwaka 2021 ijulikanayo kama Sheria ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na Usimamizi wa Mali za Umma na mambo mengine yanayohusiana na hayo baada ya kufutwa kwa Sheria nambari 4 ya mwaka 2002 Sheria ya Mitaji ya Umma.

Lengo kuu la Serilkali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuunda Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia na kutathmini utendaji wa jumla wa Taasisi za Uwekezaji, Mashirika ya Umma na makampuni ambayo Serikali ina umiliki wa hisa au kuna maslahi ya umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news