VIDEO:Madereva wa malori wasema suluhisho ni Bandari Kavu ya Kwala, wamwangukia Rais Dkt.Samia

PWANI-Madereva wa malori kutoka mataifa mbalimbali ambao wanaitumia Bandari ya Dar es Salaam kupata huduma wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kufanya maamuzi ya haraka ili kuwaondolea kadhia wanayoipata ya kukaa sehemu moja kwa muda mrefu.
Wamesema, suluhu pekee ambayo itaweza kuwaondolea kadhia hiyo kwa sasa ni kuhakikisha Bandari Kavu ya Kwala inaanza kutoa huduma.

Kwa nyakati tofauti leo Januari 17,2024 madereva hao wakiwa katika eneo la ukaguzi Misugusugu, Kibaha mkoani Pwani wamesema, ni jambo la kusikitisha wao kuendelea kukaa muda mrefu barabarani.

Wamesema, miongoni mwao wana siku 20 huku wakilala kwenye magari na wakati mwingine wanakosa chakula.
Madereva hao wamesema, wanateseka licha ya kukaa muda mrefu nje wakitolea mfano kuwa kuna waliokaa miezi miwili, mwezi mmoja na miezi mitatu.

Aidha, wamesema hadi sasa hawajui hatima yao ya kuondoka itakuwa lini.

Kwa upande wa baadhi ya Wazambia wamesema, wameleta mizigo na hawajui lini mizigo yao itashushwa na lini watarejea nchini kwao.

Wamesema, hali hiyo imeyafanya maisha yao kuwa magumu, hivyo wanaiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia kati ili waweze kupata wepesi wa ushushaji wa mizigo yao.

Wamesema kuwa,kitendo cha kufika na kukaa Misugusugu zaidi ya kilomita 60 kwa muda mrefu halafu wakashushe mizigo yao Ubungo warudi tena Zambia inawagharimu sana kiuchumi.

Madereva hao wanasema, hali zao si njema kwani wanatumia muda mwingi kulala kwenye magari, hivyo wanahatarisha maisha yao hata udereva wao unakuwa ni wa hatari.

Vile vile, madereva hao wamesema baadhi ya ajali zinazotokea barabarani zinaweza kuchangiwa na msongo wa mawazo, kuchoka na kusinzia.

Hivyo, wameiomba Serikali kuharakisha Bandari Kavu ya Kwala ili ianze kutoa huduma waweze kushusha mizigo yao hapo na kuendelea na safari.

Hayo yamejiri ikiwa ni siku mbili zmepita tangu Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa Alphonce Temba kumtaka Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kutoka hadharani na kueleza kwa nini Bandari Kavu ya Kwala hadi sasa haijaanza kufanya kazi.

Kauli hiyo ameitoa Januari 15, 2024 akizungumza na mwandishi habari hizi ambapo ameujia juu uongozi wa Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na kuhoji kwa nini walitumia fedha za Serikali shilingi Bilioni 83.246 kwa kazi ya ujenzi wa mradi huo ambao hauna mwanzo wala mwisho.

"Kila Waziri anayeingia kwenye Wizara hii, miaka nenda, miaka rudi wanaendelea kusema kwamba ndani ya miezi sita Bandari Kavu ya Kwala itaanza kufanya kazi. Taarifa zilizotoka leo tarehe 15 Mwezi wa Kwanza 2024 ni kilio cha Wafanyabiashara, kushushiwa mizigo yao na TPA," amesema Mwinjilisti Temba na kuongeza,

"Na TPA wanasema ni neema kuongezeka gati tano ili kukidhi kiu ya wateja kwa maana gati tano zaidi zitatengenezwa mwaka huu 2024 ili kukidhi kiu ya wateja. 

"TPA wamekuwa na kizungumkuti kana kwamba hawajui wanachokifanya kwa sababu leo hii nazungumzia kuhusu mrundikano na ucheleweshwaji wa kupata mizigo kwa wafanyabiashara Tanzania na magazeti mengi yamenukuliwa hivyo."

Mwinjilisti Temba amebainisha kuwa, aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Isack Kamwelwe aliagiza Julai 1, 2019 iwe siku ya ufunguzi wa mradi huo wa Bandari Kavu ya Kwala ili mizigo ianze kushushwa katika eneo hilo na Watanzania wachukue mizigo yao hapo.

"Lakini ni miaka mingi sasa imepita 2020, 2021, 2022, 2023 na hadi leo 2024 ni miaka mitano, bado Wizara ya Ujenzi na TPA kila mwaka wanasema jambo hilo hilo kwama Bandari Kavu ya Kwala itafunguliwa baada ya miezi 6," ameeleza Mwinjilisti Temba.

Kwamba aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Gabriel Migire katika taarifa yake kwa umma ya Desemba 4, 2022 kupitia kwa vyombo vya habari alisema kuwa, Bandari Kavu ya Kwala inaanza kufanya kazi.

Hata hivyo hadi leo bado haijaanza kufanya kazi na wala hakuna dalili ya kuanza kufanya kazi. Vile vila amekumbusha kuwa Oktoba 2021, Waziri Prof. Mbarawa alitoa miezi sita kwa TPA kukamilisha Bandari kavu hiyo lakini hadi leo bado.

"Hali hii imeleta shida kubwa sana kwa sababu watu wanateseka, Oktoba 2021 Rais wa Burundi alikabidhiwa eneo Kwala kwa ajili ya kuweka Bandari Kavu, mwaka jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan aliwakaribisha Wazambia na kuelekeza wapewe eneo Kwala, hiyo ilikuwa mwaka jana mpaka leo hii Bandari Kavu ya Kwala Watanzania hawajui nini kinaendelea na kwa taarifa ambazo zilitolewa na TPA huko nyuma, ilikuwa ihudumie makasha 822 kwa siku," amesema Mwijilisti Temba na kueleza,

"Hivyo kwa mwaka mzima ni makasha laki 3395, sasa makasha haya yataendelea kutolewa palepale Bandari ya Dar es Salaam, tumekuwa tukiwaambia viongozi wa nje kama Rais wa Burundi, Rais wa Zambia waende pia wajenge Kwala na maeneo wameonyeshwa, lakini bado tumeendelea kuonyesha mizigo ichukuliwe Dar es Salaam."

Mwinjilisti Temba amesema kuwa, kitendo cha Serikali, Waziri wa Uchukuzi na TPA kuendelea kukaa kimya juu ya utendaji kazi na nilini Bandari Kavu ya Kwala itaanza kufanya kazi sio jambo la busara kwani Wafanyabiashara wanaendelea kuteseka na mizigo yao, huku pia Jiji la Dar es Salaam likiwa haliingiliki wala kutoka wakati wote.

Kwamba hiyo imesababisha watu kupata shida ya msongamano na watu kufika nyumbani wakiwa wamechelewa huku zaidi ya shilingi bilioni 2 zikipotea pamoja na ndoa nyingi kuvunjika kwa sababu ya hali ya maisha kutokana na kutokufika kwa wakati na familia nyingi kuyumba.

"Hivyo basi ni wakati sasa Waziri wa Uchukuzi na TPA ituambie Watanzania Bandari Kavu ya Kwala ambayo sasa hivi haizungumziwi tena itaanza lini. Lakini niwashauri viongozi kama walishauacha mradi huu wasiuzungumzie tena na watupe ni njia gani itakayosaidia kuondoa msongamano wa Malori katikati ya Jiji la Dar es Salaam," amesema.

Amesema kwamba Watanzania waliamini kuwa mwaka huu wa 2024 ungekua ni mwaka wa utulivu kwa kumaliza msongamano wa Malori katikati ya jiji la Dar es Salaam, lakini inaonekana kama TPA wamelifumbia macho jambo hilo.

Wakati huo huo, Mwinjilisti huyo machachari amedai kusikitiswa na baadhi ya watanzania wanaomshangaa anavyotoka hadharani na kuyasemea mambo makubwa ya nchi.

Baadhi wamekuwa wakihoji yeye ni nani hadi kuwa na nguvu kubwa hivyo au nani anamtuma atoe taarifa za mambo hayo ambayo wananchi wanadai angepitia kwa Diwani au Mbunge kuwakilisha hoja zake kwanza.

Temba alisema, moja ya kazi ya kiongozi yoyote wa dini ni kuombea,kushauri na kuikemea serikali ambayo inayafanyia kazi mambo hayo kwa manufaa mapana akitoa mfano alidai mwaka 2008 alimpa ushauri aliyekuwa Waziri Mkuu wa Awamu ya Nne, Mh.Mizengo Pinda.

Ni kuhusu Serikali kujenga Mzani wa Vigwaza Kambini Bagamoyo kipindi hicho mzani huo ulikuwa Maili moja Kibaha na Serikali ikafanya hivyo kupitia Bunge la kipindi hicho.

"Hivyo kama kipindi hicho nilikuwa na uwezo wa kuwakilisha mawazo yangu hadi Bunge kuridhia na leo kukazaliwa Bandari kavu ya Kwala ni ndani ya wazo langu.

"Lakini pia Katiba ya Mwaka 1977 iko wazi kuhusu Uhuru wa maoni ambao hauingiliwi hata na maalaka ya nchi katika kutoa na kupata habari, lakini kila mtanzania ni mlinzi wa rasilimali ya nchi.

"Ijulikane zipo rasilimali,vitu,watu na pesa ambazo zinatakiwa kulindwa na watanzania wote. Tunavyoisifia Serikali ndiyo haki pia kuihoji na kuikemea,"amefafanua Mwinjilisti Temba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news