BoT:Kuendesha kikundi cha kukopeshana bila usajili faini na jela inakuhusu

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa, kwa mujibu wa Sheria Ndogo ya Huduma za Fedha (The Microfinance Act,2018) imeweka wazi kuwa, mtu yeyote atakayebainika kuendesha kikundi cha kuweka na kukopeshana fedha bila kibali atatozwa faini ya shilingi milioni 10 au kifungo cha miaka miwili hadi mitano jela.

"Mtu anayebainika kuendesha kikundi (vikundi vya kukopeshana) bila kuwa na usajili kwa mujibu wa Sheria Ndogo ya Huduma za Fedha (2018) kifungu cha 16 (4), sheria inasema kutakuwa na faini isiyopungua shilingi milioni 10, kifungo cha miaka miwili mpaka mitano au vyote kwa pamoja.

"Pia kama kikundi hakina usajili rasmi wa Serikali hakiwezi kupewa mkopo na taasisi yoyote, kununua mfano ardhi au kushirikishwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo, hivyo ni muhimu wananchi kuhakikisha wanasajili vikundi vyao ili waweze kuvitumia kujiletea maendeleo huko walipo;
Hayo yamesemwa leo Februari 15, 2024 na Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Sekta ya Fedha-Idara ya Usimamizi wa Huduma Ndogo ya Sekta ya Fedha BoT, Deogratius Mnyamani.

Ni katika siku ya pili ya semina kwa waandishi wa habari za uchumi iliyoandaliwa na BoT ambapo amewasilisha mada ya maendeleo ya utekelezaji wa Sheria Ndogo ya Huduma za Fedha (The Microfinance Act.2018).

Mbali na hayo amesema, ujio wa Sheria Ndogo ya Huduma za Fedha (The Microfinance Act,2018) imekuwa msingi muhimu katika kudhibiti wakopeshaji wa mikopo holela na kuweka uwazi ili wananchi wanaokopa waweze kupata mikopo kuendeleza miradi yao kujiletea maendeleo.

Sheria hiyo imeipa Benki Kuu ya Tanzania jukumu la usimamizi wa watoa huduma ndogo za fedha waliogawanyika katika madaraja manne.

Amesema, daraja la kwanza linajumuisha benki za huduma ndogo za fedha (microfinance banks). Daraja la pili amesema ni watoa huduma ndogo za fedha wasiopeleka amana.

"Toka sheria hii ilipoundwa hadi kufikia Februari 9, 2024 Benki Kuu ilikuwa imepokea maombi 2,274 na kutoa leseni 1,656 kwa watoa huduma za fedha wa daraja la pili waliokidhi vigezo,"amefafanua Bw.Mnyamani.

Mnyamani ametaja daraja la tatu kuwa ni vyama vya ushirika wa akiba na mikopo huku daraja la nne likiwa ni vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha. "Kwa upande wa SACCOS,Tume ya Maendeleo ya Ushirika imepokea jumla ya maombi 1,215 na kuidhinisha leseni 884 kwa SACCOS zilizokidhi vigezo."

Amesema, kwa upande wa vikundi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI ) imepokea jumla ya maombi 49,910 ya usajili wa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha ba kutoa hati za usajili kwa vikundi 48,826.

"Haya madaraja yote yanatakiwa yasimamiwe na Benki Kuu kwa mujibu wa sheria, lakini pia sheria hii imeipa mamlaka Benki Kuu kukasimisha madaraka kwa mfano Tume ya Maendeleo ya Ushirika inasimamia Saccos huku Mamlaka za Serikali za Mitaa ikikasimishwa madaraka ya kusimamia vikundi.

"Sheria inasema, licha ya kukasimishwa madaraka Benki Kuu inaweza kwenda moja kwa moja kwenye hayo maeneo, na kutoa miongozo, mafunzo, kutengeneza miundo, hivyo Benki Kuu ina jukumu la kuwapa mafunzo waliokasimiwa madaraka, kwa hiyo chochote kitakachokuwa kinafanyika, kitakuwa kwa niaba ya Benki Kuu."

Mnyamani amefafanua kuwa, Serikali imekuja na sheria hiyo ili kuhakikisha mikopo inayotolewa na huduma ndogo za fedha nchini inakuwa na manufaa kwa wananchi na bila kuwaumiza.

"Mambo ya kukopeshana yamekuwepo hata kabla ya kuja kwa Yesu, kwa hiyo hizo biashara zilikuwepo. Kwa hiyo mambo yamekuwa yakienda ndivyo sivyo, kutokana na ukopeshaji holela.

"Kwa sababu kulikuwa hakuna sheria ambayo ilikuwa inadhibiti huduma ndogo ya fedha nchini.

“Moja wapo ya changamoto zilizoonekana wakati ule, ni kutokuwepo kwa uwazi wa kutosha, watu wanakopeshana bila kujua kwa kina nini kilichopo katika ule mkataba wa kukopesha. Haujui, wewe umechukua tu mkopo,

“Tuna kesi mtu baada ya kukopa milioni tatu ndani ya mwaka inageuka kuwa milioni 70, hizo milioni 70 zimetoka wapi?.

“Watu walikuwa wanatozana riba kubwa, na watu walikuwa hawana uwezo wa kulipa deni, lakini pia kumekuwa na ukopeshaji holela, mtu anakuja na kikararasi robo page anakusainisha anasema huo ni mkataba.

“Kumekuwa na malimbikizo ya madeni pia, kwa sababu watu wanachukua mikopo kiholela bila kuwa na malengo, hivyo kuwa na madeni mengi.

“Hivyo, ilionekana kuna haja ya kuwa na sheria na taratibu ili kuweza kutambua mtu anapokopa na kukopesha, kufahamu historia yake ya ukopaji. Na tumesikia wanaoumia sana ni wanawake,"amesema Mnyamani huku akisisitiza kuwa, wanaendelea na jitihada kubwa za kutoa elimu.

Amesema, Benki Kuu imeendelea kutoa elimu kwa kila kanda kwa watoa huduma ili waweze kutambua majukumu yao waweze kutoa huduma sahihi na bora kwa wananchi.

Fahamu

Novemba 23, 2018 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 (The Microfinance Act, 2018) kwa upande wa taasisi za kifedha zisizokuwa za kibenki ili kutekeleza matakwa ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017.

Ibara ya 12 ya sheria hiyo imeipa mamlaka Benki Kuu ya Tanzania kusajili, kusimamia na kudhibiti biashara ya huduma ndogo za fedha Tanzania Bara.

Vile vile, sheria hiyo imetoa tafsiri ya huduma ndogo za fedha kuwa ni biashara inayojumuisha kupokea fedha, kama amana au riba kutokana na amana au mkopo na kuikopesha kwa wanachama au wateja, kupokea amana na kutoa mikopo au huduma ya mikopo kwa wajasiriamali wadogo, kaya au mtu mmoja mmoja.

Pia,kutoa huduma za mikopo midogo, akiba ndogo, bima ndogo, huduma ndogo za karadha, pensheni ndogo na mikopo midogo ya nyumba, huduma za kutuma fedha na malipo, ikijumuisha huduma ndogo za fedha kwa njia ya mtandao.

Vile vile kutoa elimu ya fedha na huduma nyingine zinazofanana na hizi kama zitakavyoainishwa kwenye Kanuni za Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2019.

Kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 taasisi zinazoruhusiwa kutoa huduma za kifedha na mikopo nchini ni pamoja na umoja wa kusadiki, kampuni za mikopo,ushirika (Saccos),kampuni za bima, mifuko ya hifadhi ya jamii na watu binafsi nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news