Mkurugenzi Mtendaji wa Redio Penuel Fm, Mwinjilisti Temba avunja ukimya kuporomoka kwa maadili tasnia ya habari nchini

DODOMA-Mkurugenzi Mtendaji wa Redio Penuel FM mkoani Kilimanjaro ambaye pia ni Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba katika Mkutano wa Mwaka wa Watoa Huduma wa Sekta ya Utangazaji ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete ameibuka na mambo makubwa ndani ya hoja alizoziibua.

Akifafanua mambo hayo nje ya mkutano huo, Mwinjlisti Temba amesema kuwa, alipata nafasi mara mbili ya kuchangia maoni yake katika mkutano huo na alijikita wazi na kueleza mengi na ya muhimu katika kuendeleza tasnia hiyo kutokana na mada zilizokuwa zimewekwa mezani ikiwemo mada ya maadili pamoja na mambo ya kiteknolojia hususani kuhusu mitandao ya kijamii.
Kwamba katika Mkutano huo wa siku mbili ulioanza Februari 13, 2024 na kutamatika Februari 14, 2024 ambao ulijumuisha wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, wamiliki wa vyombo vya habari na watu wa cables wakijadili mambo mbalimbali kuhusu maadili na mustakabali wa tasnia hiyo, Mwinjilisti Temba alieleza wazi kuwa kuna mambo yanayotakiwa kufanyiwa kazi kutokana na kuporomoka kwa maadili na uandishi wa habari usiofuata misingi nchini pamoja na mambo mengine ya tasnia hii ya habari.

Hivyo Mwinjilisti Temba katika hilo amesema kuwa tatizo kubwa katika Nchi ya Tanzania ni pale lugha zetu ambazo ni sehemu ya baraka ya Mwenyezi Mungu tulipozipuuza kwa kuona kwamba watu wanaoziheshimu na kuzitumia hadharani ni kama watu ambao ni wakabila.

Amesema ndiyo maana hata sasa zaidi ya asilimia 70 ya waandishi wa habari vijana, hawajui lugha zao yaani lugha ya baba na mama zao ambapo amesema faida iliyokuwepo kwenye lugha hizo zikiwemo lugha za Kichaga, Kimasai, Kisukuma, Kinyakyusa, Kiha, Kinyamwezi, Kigogo, Kikuria, Kihaya na kadhalika zilikuwa ndani ya maadili makubwa.

"Ambayo wazazi wetu, ambao wengi wao mababu na mabibi hawakusoma kabisa, lakini zilikuwa na taratibu za heshima kati ya watu na watu, taratibu ya nidhamu, taratibu ya utu, lakini pale tulipozibomoa lugha hizi ndiyo tulipokosea," amesema Mwijilisti Temba.

Hivyo Mwinjlisti Temba ameshauri vyombo vya habari kurudisha tamaduni zetu ikiwemo kuwa na vipindi katika kila Mkoa na Wilaya ambapo Radio hizo zipo na waite Wazee katika vipindi hivyo ili wazungumzie shuhuda za maisha walivyokuwa wakiishi kwa maadili.

"Mfano Kilimanjaro ambako kuna kitu kinaitwa Mviyaho, Kichaga mana yake laana ambazo asilimia kubwa ya vurugu kubwa zinazowatesa watu wa Moshi ni pale wanapoachiana laana hovyo, na laana zinaachwa kwasababu ya taratibu ya mila zinazokiukwa hususan migogoro ya ardhi na kadhalika na mambo mengine ambayo wamefikia hatua watu kutamkiana laana na kulaani familia, laana hizo hufanya kazi na kuathiri wengi.
"Lakini wale wazee wa zamani walikuwa wakiweka mambo sawa, kama kulikuwa na mgogoro ilibidi familia zikae, kukawa na adhabu za kupigwa faini ya mbuzi, ng'ombe, chakula na kadhalika na kupatanishwa, hivyo kuondoa migogoro na laana juu ya maisha yao."

Kwamba katika makabila mengi watu wanaishi bila kujua taratibu ya mila zao, hivyo matokeo yake ndiyo waandishi wa habari wa sasa ambao wamekuwa wakichukua maudhui katika YouTube kwenye tamaduni za Ulaya, Magharibi na Nchi Mbalimbali.

Hivyo wanapoyaingiza kwenye tamaduni za Tanzania ndipo tunapata vitu vya hovyo, ikiwemo wasanii kuharibika na hivyo kuchochea mmomonyoko wa maadili na kutokuwa na uadilifu.

"Halafu tunawategemea wasanii hawa ambao kila siku wanawapa mimba dada zetu kila siku wanawaacha na tunawategemea watuongoze. Jambo hili limekuwa ni janga sana kwa nchi yetu."

Hata hivyo Kamati ya Nidhamu ya TCRA ilikiri kwamba wamekuwa wakipambana na watu wengi ambao wamekuwa wakiwasumbua wakiweka wazi kuwa ni watu kutoka vyombo vikubwa na wasanii wakubwa ambao hata ambapo wamekuwa wakiwaita na kuwaonya bado wamekuwa wakirudia kitu hicho hicho.

Kwamba jambo hilo ni kiashiria kuwa kiwango cha kuporomoka kwa maadili kimekuwa kikubwa.

Aidha, kwenye mada ya kuhusu wasanii wa muziki, wachangiaji katika mkutano huo waliwasifia wasanii hao kwamba wamekuwa wakisasa na wamekuwa wakifanya vizuri ambapo katika mada hiyo ni watu wawili tu walichangia na kueleza wanavyolidhishwa na kazi za wasanii hao.Tazama video hapa chini;
Hata hivyo juu ya mada hiyo Mwinjilisti Temba aliandika kimemo kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo kutaka kupata majibu ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) juu ya kuachwa kwa nyimbo za Wasanii ambazo ziko kinyume na maadili ya Kitanzania.

Hivyo baada ya kuandika kimemo hicho alipatiwa muda na meza kuu kwa ajili ya kuchangia juu ya mada hiyo.

Mwinjilisti Temba aliwataja hadharana baadhi ya Wasanii wanaoimba nyimbo za kihuni ambazo ni kinyume na maadili ya Mtanzania kua ni Diamond, Zuchu na Rayvan, kwamba nyimbo zao zimekuwa zikiharibu vijana na watoto.
Hata hivyo BASATA walieleza kuwa tayari wameshatunga sheria, kanuni na taratibu zinazodhibiti wasanii kutunga nyimbo zisizofaa katika maadili ya Kitanzania.

Kutokana na tatizo hilo kukithiri, Mwinjilisti Temba ameeleza kuwa atashaurina na wanasheria wake ili kupata tafasili ya maadili yetu yanayoharibika na yanayotajwa katika Katiba na Haki za Binadamu ili Mahakama Kuu iwape tafasiri kama nyimbo za namna hiyo zinafaa kuendelea kusikilizwa hususan na watoto wadogo, ama nyimbo hizo zipigwe marufuku kwa Mahakama kuzuia nyimbo hizo za kihuni ambazo zimekuwa zikiimbwa na wasanii hao na kuharibu jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news