Mwinjilisti Temba amuangukia tena Rais Dkt.Samia kuhusu Bandari Kavu ya Kwala

DAR ES SALAAM-Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha nia njema ya kuanza kufanya kazi kwa Bandari Kavu ya Kwala mkoani Pwani.
Mwinjilisti Temba (katikati) anasema ni miongoni mwa Watanzania ambao wanavutiwa zaidi na uongozi wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda katika kushughulikia kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi kwa ustawi bora wa jamii na Taifa kwa ujumla.

Mbali na pongezi amemuomba Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kuidhinisha fungu la fedha ili liwezeshe kujenga magodauni katika bandari hiyo ambayo yatatumika kupokea Copper kutoka Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

"Lakini, juhudi za haraka kwa Serikali kuonesha ni namna gani inatatua tatizo la msongamano wa malori jijini Dar es Salaam bado ni mtihani mkubwa.

"Kwa sababu shida kubwa inayosababisha kuwepo msongamano huo ni kutokana na Serikali chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuendelea kuchapa kazi na kuifungua nchi kiuchumi, hivyo kusababisha ongezeko kubwa la malori kuongezeka sana kwa mwaka huu.

"Hivyo, mzigo mkubwa wa Copper kuongezeka, hali inayosababisha malori yanayosafirisha mizigo hiyo kuendelea ku-stuck maeneo ya Misugusugu Check Point Kibaha na pale Ubungo Bandari Kavu ambako sasa ndipo madereva wengi walikuwa wakilalamika kwamba zaidi ya malori 700 ambayo yame-stuck maeneo ya Misugusugu yanaruhusiwa takribani magari saba kuja kushusha mzigo wa Copper

"Kwa hiyo, Bandari Kavu ya Kwala kwa wale wasiokuwa na uelewa haitaweza kupokea Copper kwa sasa, kwa sababu hakuna magodauni ya kuweza kuhifadhi, kwa sababu Copper haiwekwi kwenye makontena wala nje, inapaswa kuingizwa ndani ya magodauni.

"Kwa kukosa magodauni pale Kwala kutasababisha bado uwezekano wa kushushwa kwa Copper na kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam kuwa kitendawili.

"Kwa sababu ujenzi ambao utaanza sasa hivi, unaweza kuchukua zaidi ya mwaka mmoja kukamilika, hivyo kuendelea kuonesha bado kutakuwa na shida.

"Katika haya mambo ninayozungumza ni ule ujenzi ambao fedha zimekwishapatikana, lakini mpaka sasa hivi hakuna fedha ambazo zimepatikana kwa ajili ya kujenga magodauni ili Copper inayotoka Zambia na Congo iweze kushushwa.
"Hivyo,ninamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan kuingilia kati ili kuweza kuidhinisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa magodauni ya kupoka Copper.

"La si hivyo, itakuwa bado ni stori ndefu na ndoto ya Abunuwasi kuweza kudhibiti malori kuingia katika Bandari Kavu ya Ubungo ili kushusha hizo Copper.

"Na msongamano wa malori zaidi ya 700 ambayo yapo pale Misugusugu unaendelea kuongezeka na foleni ya Ubungo haitakoma kwa sababu magodauni yanatakiwa kwa haraka ili kuweza kuishusha hiyo Copper katika magodauni hayo.

"Kwa kukosa magodauni kule Kwala hakutawezekana mzigo wowote wa Copper kutoka Zambia ukashushwa Kwala kwa sasa na mpaka sasa hivi Serikali haijasema ina kiasi gani cha fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huo, hivyo zoezi hilo linaweza kuchukua muda mrefu;

Mwinjilisti Temba ameyasema hayo leo Februari 11,2024 wakati akielezea namna ambavyo amefarijika baada ya kuona Serikali imesikia kilio cha muda mrefu cha madereva wa malori wanaosafirisha bidhaa ndani na nje ya Tanzania.

Sambamba na mrundikano wa malori katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

"Hatimaye Serikali imekuja na majibu kwamba Bandari Kavu ya Kwala tayari imekwishaanza kupangiwa mizigo kwa ajili ya kushusha makasha ikiwa ni zaidi ya asilimia 60 ya mizigo inayokwenda nje ya nchi."

Amesema, nchi hizo zinakadiriwa saba hususani zinazotuzunguka. Pia, imeelezwa kuwa baadhi ya nchi ambazo mizigo hiyo inaenda huko zimepewa nafuu na Serikali.

Ni pamoja na kupewa maeneo ya kuweka mizigo yao pembezoni mwa Bandari Kavu ya Kwala hasa panapojengwa viwanda zaidi ya 200 na Wachina.

Mwinjilisti Temba amesema, kutokana na jitihada hizo za Serikali zinakwenda kufungua fursa kubwa za kiuchumi na ajira kwa Watanzania.

Amebainisha kuwa, fursa hizo zitatokana na shughuli za viwandani, Bandari Kavu ya Kwala, vitega uchumi mbalimbali karibu na maeneo hayo.

"Hiyo ni hatua muhimu ambayo itawawezesha Watanzania wengi kuinuka kiuchumi wakiwemo wa Kwala na kwingineko.

"Pia, Watanzania wengi kupata kazi hususani wasomi ambao wamemaliza vyuo mbalimbali nchini.

"Nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa kuona uharaka huo, na kuamua kujikita sasa kwa ajili ya kuifungua rasmi Bandari Kavu ya Kwala ili iweze kutumika na kusaidia kuondoa msongamano wa malori jijini Dar es Salaam.

"Ni matumaini yangu kuwa, juhudi hizi zinakwenda kuleta hamasa kubwa ya maendeleo, kwani pia tunatarajia kuona ujenzi wa barabara kutoka Vigwaza hadi Kwala yenye urefu wa zaidi ya kilomita 15.5.

"Zote hizo ni jitihada za kuimarisha bandari kavu ambayo imeanza kufunguliwa rasmi kwa kupelekwa mizigo na baadhi ya magari kuruhusiwa kwenda kuibeba.

"Hakika, jambo hili ni la kupongezwa sana, Serikali iendelee kuimarisha juhudi zake hizo ambazo inaaminika kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt.Samia Suluhu Hassan ni Serikali inayotekeleza kwa vitendo zaidi na si hadhithi."

Vile vile, Mwinjilisti Temba ameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa malori ambao wana maeneo mengi katikati ya Jiji la Dar es Salaam ili waweze kuchangamkia fursa iende sambamba na upelekaji wa mizigo hiyo maeneo ya Kwala.

"Hili kusiwe na malori yanakaa Dar es Salaam wakati mizigo inabebwa Kwala na inaenda nje ya nchi.Kunatakiwa elimu, kunatakiwa uhamasishaji, Serikali itoe."

Amesema, "Na kama yapo maeneo eneo la Narco hususani pembezoni mwa Barabara ya Morogoro pale mpakani na Reli ya kuelekea Tanga, Kijiji cha Ruvu kuja Vigwaza kwa Zoka eneo lille lipo barabarani ambalo Narco hawalitumii, limekuwa ni msitu mkubwa ambalo wanajificha majambazi wamekuwa wakikamatwa pia Wasomali mbalimbali na Waethiopia wanaojificha kwa sababu lipo pembezoni mwa barabara.

"Na eneo hilo halitumiki kwa sababu Narco ni eneo la ufugaji kwa asilimia kubwa na mifugo huwa hairuhusiwi kulishwa pembezoni mwa barabara ya lami kwa sababu ya uharibifu pamoja ba kugongwa, hivyo eneo hilo limekuwa siyo malisho ya wanyama.

"Hivyo, Serikali kama ilivyoweza kufanya utaratibu wa kuweza kulitoa eneo la Mtupila lililoko Narco kwa ajili ya kutengeneza mzani wa upimaji wa malori na check point ya TRA ambayo imekamilika kwa miaka miwili sasa.

"Ndiyo hivyo hivyo Serikali ingetoa eneo hilo la mwanzoni mwa Narco karibu na Ofisi za Narco kuja kwenye reli ya treni pembezoni mwa barabara ili kuwakodisha wenye malori, kuwakatia hekari mbili au tano kwa kila wamiliki wa malori kutokana na malori yao ili waweze kupata fursa ya kuweza kukodisha, hatua ambayo pia itaongeza kipato kwa Narco.

"Shirika ambalo limeendelea kuwa hoi kutokana na changamoto ya kuendelea kupungua kwa wanyama, vifaa vyao kwa maana ya matrekta, magari ambayo yamekuwa yakichoka hivyo kuegeshwa bila kufanya kazi.

"Hivyo, ninaishauri Serikali bado ina kazi kubwa sana ikiwemo kuangalia namna ya kuhamisha Misugusugu Check Point kwa maana ya TRA kuhama hapo na kwenda Vigwaza kambini ambako majengo yao yamekwisha kamilika zaidi ya miaka miwili sasa.

"Na maegesho yamekwisha kamilika zaidi ya miaka miwili sasa, matokeo yake jengo na eneo la maegesho linapigwa jua na kuendelea kukatika katika kwa sababu hakuna uengeshaji wowote unaendelea pale.

"Kwa hiyo, tunaendelea kushangaa kwa nini mpaka sasa hivi TRA inaendelea kung'ang'ania pale Misugusugu Check Point.

"Sehemu ambayo haina miundombinu, barabara ni mbovu, malori yanakata springs chini kwa sababu ya mabwawa ya maji ndani ya eneo hilo la Misugusugu Check Point.

"Huku eneo ambalo limejengwa na TRA na Serikali kwa ajili ya Check Point, Vigwaza Kambini kwenye eneo la mzani bado wakiwa hawajahamia.

"Ninaishauri Serikali kufanya haraka kuhamia kwenye eneo lile, kitendo cha kuhamia pale kitasaidia akina mama na vijana wengi kupata fura za ajira.

"Wengine watakuwa mama lishe maeneo yale, kuuza vyakula kwa ajili ya hao, lakini hata vijana ambao wengi wamejikita katika kukata mikaa maeneo hayo ya mashamba ya Narco wataacha kukata mikaa na watafanya biashara ndogo ndogo."

Amesema, biashara hizo ni pamoja na kuuza maji, vyakula, kutembeza korosho na biashara nyingine halali.

Pia, Mwinjilisti Temba amesisitiza kuwa, biashara hizo zitawapa vipato tofauti na kuharibu maliasili na kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa.

Uchomaji mkaa huo, Mwinjilisti Temba amesema, umeendelea kuchangia madhara makubwa katika mazingira ikiwemo kusababisha jangwa nchini.

"Ukiangalia sasa hivi kutokana na uharibifu wa mazingira hasa Ukanda wa Pwani joto limekuwa juu sana, kwa sababu miti mingi imekuwa ikikatwa holela kwa ajili ya uvunaji wa mkaa."

Amesema,Serikali ina wajibu mkubwa kwani suala la kuhamia Kwala linaendana sambamba na magodauni.

"Kwa sababu kitendo cha kuhamia Kwala kitaonesha tu ni mizigo ile ambayo inaenda nje ya nchi kupelekwa pale na kusombwa, lakini bado tatizo kubwa ambalo lipo sasa hivi hasa jijini Dar es Salaam pale kwenye Bandari Kavu ya Ubungo halitakuwa limeguswa wala kuisha.

"Na linaweza kuchukua zaidi ya mwaka mzima kuanzia sasa kukamilika kwa sababu Bandari Kavu ya Kwala sasa hivi inaonekana ni mizigo ya makontena yanapelekwa kutoka Bandarini ili yabebwe yapelekwe nchi mbalimbali ambazo makasha hayo yanakwenda,"amesisitiza kwa kina Mwinjilisti Temba.

Mwinjilisti Temba pia, ameiomba Hahlmashauri ya Chalinze iharakishe kupima mji wa Kwala, Vigwaza, Mbala Chamakweza, Mperamumbi,Gwale ,Gwata na Chauwa kwa kuwa watu wengi watahamia huko ili kusiwe skwata.

"TPA ikumbuke kufungua njia ya kurudisha makontena yanayorudi kutoka nje ya nchi, hivyo kufunguliwe njia kuanzia Msolwa,Chauwa ,Gwata,Gwale, Mperamumbi kutokea Kwala Bandari kavu.

"Njia hiyo ipo ya Mkoloni na TPA wanaifahamu hili kusiwe na tegemeo la njia moja kuna zaidi ya malori laki moja nchini yanayosafirisha mizigo,"amesema Mwinjilisti Temba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news