Serikali kuyaendeleza makazi ya Mwalimu Nyerere

MARA-Serikali imedhamiria kuyafanya makazi ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyoko kijiji cha Mwitongo, wilayani Butiama mkoani Mara kuwa kituo cha utalii.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiweka akiwasha mshumaa kwenye kaburi la hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mwitongo, Butiama mkoani Mara Februari 27, 2024.

Hayo yalisemwa Jumanne, Februari 27, 2024 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wakazi wa Kitongoji cha Muhumba, wilayani Butiama, akiwa njiani kuelekea Mugumu, Serengeti ambako anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Mara.

Waziri Mkuu Majaliwa alimwagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Moses Kaegele atembelee eneo, akagua na kuangalia mapungufu yaliyopo ili Serikali iweze kuyafanyia kazi. Pia ameiagiza wizara ya ujenzi ishughulikie barabara ya kutoka Serengeti hadi Butiama ili ikamilike na kuwawezesha watalii wanaotaka kufika kwenye makumbusho hayo kwa njia ya barabara.

Waziri Mkuu alipitia Mwitongo na kuwasalimia wanafamilia wa Baba wa Taifa na kuweka shada la maua kwenye kaburi lake.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye kaburi la hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mwitongo, Butiama mkoani Mara Februari 27, 2024.

Mapema, alipowasili wilayani humo, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama ambayo utekelezaji wake umefikia asilimia 60.

Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe hilo, Waziri Mkuu alimtaka mkandarasi wa mradi huo ambaye ni Wakala wa Majengo (TBA) ahakikishe anaukamilisha mradi huo kwa wakati. Hadi sasa, mkandarasi ameshalipwa sh. milioni 843.4 ikiwa ni malipo ya awali na hati za malipo ya pili na tatu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji ambapo kazi kubwa imefanyika na sasa nguvu kubwa inaelekezwa kwenye kufikisha umeme kwenye vitongoji.

Akizungumza na wakazi wa Issenyi, wilayani Serengeti, akiwa njiani kuelekea Mugumu, Mheshimiwa Majaliwa alitoa rai kwa Watanzania waachane na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake waanze kutumia gesi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news