Waziri Mkuu kufanya ziara ya kiserikali mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa anatarajia kufanya ziara rasmi ya Kiserikali mkoani Mara kuanzia Februari 25, 2024 hadi Februari 29, 2024.
Hayo yamebainishwa Februari 24, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Said Mohamed Mtanda wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Musoma akielezea ujio wake.

Mheshimiwa Mtanda amebainisha kuwa, Waziri Mkuu katika ziara yake mkoani humo atazungumza na watumishi, viongozi, kufanya mikutano ya hadhara, kutembelea miradi, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika katika sekta mbalimbali.

Miongoni mwa sekta hizo ni pamoja na sekata za elimu, utawala, miundombinu pamoja na sekta ya afya.

Huku akiwaomba kwa dhati wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya hadhara ambayo ataifanya.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema,mapokezi ya Waziri Mkuu Majaliwa yatafanyika eneo la Ndabaka, Wilaya ya Bunda mnamo Februari 25, 2024 mchana na baada ya hapo ataelekea Ukumbi wa Uwekezaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara ili kupokea taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Mara

Ambapo Februari 26, 2024, Waziri Mkuu Majaliwa atasalimia wananchi eneo la Mariwanda kabla ya kutembelea na kukagua Shule ya Msingi Sabasita iliyopo eneo hilo, atakagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Mara Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani humo.

Baada ya hapo Waziri Mkuu Majaliwa atakagua na kuzindua mradi wa maji wa Sazira pamoja na kufanya kikao na watumishi na viongozi na baadaye kufanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Msingi Miembeni, Bunda Mjini ambapo wananchi wameombwa kujitokeza kwa wingi.

Na Februari 27,2024 Waziri Mkuu Majaliwa atakagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, kufanya kikao na watumishi na viongozi, Kisha kuwasalimia wananchi wa Butiama na kutembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere eneo la Mwitongo wilayani Butiama.

Pia, Waziri Mkuu Majaliwa atafanya kikao na watumishi na viongozi Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Sokoine uliopo Mugumu na baadaye kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Getarungu wilayani humo.

Baadaye Waziri Mkuu Majaliwa atakwenda eneo la Nyamwaga na ataweka jiwe la msingi katika jengo la utawala Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kusalimiana na wananchi katika eneo hilo la Nyamwaga.

Februari 28, 2024 Waziri Mkuu Majaliwa atatembelea na kukagua mradi wa maji Komuge na baadaye kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kabla ya kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la Utegi Wilayani humo.

Baadaye Waziri Mkuu Majaliwa atafanya mkutano wa hadhara katika eneo la Sirari na kwenda kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa soko la kimkakati la Mji wa Tarime na kufanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Serengeti katika Mji wa Tarime.

Februari 29, 2024 Waziri Mkuu Majaliwa atakagua ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma na baadaye ataelekea kijiji cha Suguti kuweka jiwe la msingi katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Musoma pamoja na kuongea na viongozi na watumishi wa halmashauri hiyo.

Pia, Waziri Mkuu Majaliwa atakwenda Kijiji cha Bwai (Bwai Kumsoma) kwa ajili ya kuzungumza na wananchi wa Bwai na atahitimisha ziara yake katika Manispaa ya Musoma ambapo atafanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Sekondari Mara ambapo Wananchi wameombwa kujitokeza kwa wingi kumsikiliza kiongozi huyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Said Mohamed Mtanda amesema kuwa, Mkoa wa Mara ni salama na hali ya ulinzi na usalama imeimarishwa vyema, hivyo Wananchi wajitokeze kwa wingi na kwa upendo katika maeneo ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa atafanya mikutano ya hadhara kuzungumza nao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Rorya hatuna zao la kudumu la biashara, ila zao la TUMBAKU linafanya vizuri Sana Rorya lakini tatizo kubwa hatuna mnunuzi WA zao Hilo hapa Rorya. Je, utatusaidiaje Ili mnunuzi/Wanunuzi wapatikane hapa Rorya?

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news