Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa afariki

NA GODFREY NNKO 

WAZIRI Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Edward Lowassa amefariki dunia, akiwa anapatiwa matibabu jijini Dar es Salaam.

Lowassa alikuwa Waziri Mkuu wa Tisa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipokea nafasi hiyo kutoka kwa Mheshimiwa Fredrick Tluway Sumaye.

Alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia Desemba 30, 2005 hadi Februari 7, 2008 alipojiuzulu na hatimaye kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri. Alikifuatiwa na Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda.
Tangazo la kifo cha Lowassa limetangazwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango.
Katika tangazo fupi alilolitoa kupitia televisheni ya taifa, Mpango amesema kuwa Lowassa amefikwa na umauti katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameeleza kupokea kwa mshutuko taarifa za kifo cha Edward Lowassa,

"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa. 

"Mheshimiwa Lowassa ameitumikia nchi yetu katika nafasi mbalimbali kwa zaidi ya miaka 35, akianzia ushiriki wake katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge, Waziri katika wizara mbalimbali na Waziri Mkuu. 

"Tumempoteza kiongozi mahiri, aliyejituma na kujitoa kwa nchi yetu. Natoa pole kwa mjane, Mama Regina Lowassa, watoto (Mheshimiwa Mbunge wa Monduli, Fredrick Lowassa na wadogo zako), ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mzito. 

"Katika mawasiliano yangu na familia, nimewaeleza kuwa kama taifa tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu, na kamwe wasiache kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutafakari neno lake, hasa Kitabu cha Ayubu 1:21.Mwenyezi Mungu amweke mahali pema. Amina,"amefafanua Rais Dkt.Samia.
Edward Ngoyai Lowassa
Mbunge
Bunge laTanzania
Jimbo la uchaguziMonduli (Arusha)
Tarehe ya kuzaliwa26 Agosti 1953
Tarehe ya kifo10 Februari 2024
ChamaCCM (tangu 01/03/19)
Tar. ya kuingia bungetangu 1990
Alirudishwa mwaka2005
Waziri Mkuu wa Tanzania
Alingia ofisini2005
Alitanguliwa naFrederick Sumaye
DiniMkristo
Elimu yakeChuo Kikuu
Digrii anazoshikaMA (Development Studies) University of Bath (Uing.)
Kazimwanasiasa
Nafasi alizowahi kuhudumu kama mtumishi wa umma kwa nyakati tofauti nchini;
NafasiMwaka
Waziri Mkuu2005–2008
Mbunge wa Jimbo la Monduli1990–2015
Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo2000–2005
Waziri wa Nchi, Mazingira na Mapambano dhidi ya Umasikini (Ofisi ya Makamu wa Rais)1997–2000
Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi 1993–1995
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (Haki na Masuala ya Bunge)1990–1993
Mkurugenzi Mtendaji wa Arusha International Conference Centre (AICC)1989–1990

Aidha, mwaka 2014 Edward Lowassa alisimamishwa na Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kushtakiwa kwamba aliwahi kuanzisha kampeni ya kuwa mgombea wa urais kabla ya kipindi kilichokubaliwa na chama hicho

Mei 2015,alianzisha kampeni yake rasmi,lakini kamati kuu ya CCM ilimuondoa katika orodha ya majina yaliyopelekwa kwa uteuzi ndani ya chama.

Lowassa aliondoka CCM na Julai 28, 2015 alijunga rasmi na chama cha upinzani cha CHADEMA.

Siku chache baadaye aliteuliwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CHADEMA mnamo Oktoba 2015. 

Kwa mujibu  wa Tume ya Uchaguzi alishindwa kwa kupata asilimia 39.97 za kura zote na mgombea wa CCM, ambaye kwa sasa ni marehemu, Dkt. John Pombe Magufuli aliyepata asilimia 58.46 ya kura.

Licha ya kushindwa kutimiza ndoto ya urais, Lowassa aliendelea kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA. 

Ingawa, Januari 2018 alifanya mazungumzo na Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, bila kujua kilichojadiliwa Machi Mosi,2019 alirejea tena Chama Cha Mapinduzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news