Yanga mmefanya kweli,Robo fainali dili

NA LWAGA MWAMBANDE

CHINI ya Kocha Miguel Ángel Gamondi, Yanga SC ya jijini Dar es Salaam imepata ushindi wa kushangaza dhidi ya CR Belouizdad kutoka Algeria.
Ni katika mchezo wa Kundi D Ligi ya Mabingwa barani Afrika ambao umepigwa usiku huu.

Mtanange huo wa nguvu umepigwa leo Februari 24,2024 katika Dimba la Benjamin Mkapa katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Mabao hayo yamewekwa nyavuni na Mudathir Yahya Abbas dakika ya 43, Stephane Aziz Ki dakika ya 47.

Mengine yamefungwa na Kennedy Musonda dakika ya 48 na Joseph Guede Gnadou dakika ya 84 ya kipindi cha pili cha mchezo huo.

kwa matokeo hayo Yanga inafikisha alama nane na kusogea nafasi ya pili ikiwa ni nyuma ya mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri baada ya wote kucheza mechi tano.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande licha ya kuwapa kongole Yanga SC kwa matokeo hayo, pia amesema wametinga kibabe kwa kuwakomesha Waarabu. Endelea;

1.Yanga mmefanya kweli, hongera hongera kweli,
Robo fainali dili, mmeingia kamili,
Siyo taa ya kandili, wenu mwanga ni mkali,
Mlivyotinga kibabe, hakika mmekomesha.

2.Tena hao Waarabu, mmewasigina kweli,
Waondoka na aibu, kapu hilo la magoli,
Sasa muda kuratibu, mechi robo fainali,
Mlivyotinga kibabe, hakika mmekomesha.

3.Mmeing’arisha Yanga, sasa robo afadhali,
Tanzania tunaringa, tuko robo fainali,
Na karata tukichanga, na Simba haiko mbali,
Mlivyotinga kibabe, hakika mmekomesha.

4.Heko kwenu wachezaji, mmepambana kikweli,
Makocha wa wachezaji, mnajiweza kamili,
Viongozi washikaji, hongera kufika mbali,
Mlivyotinga kibabe, hakika mmekomesha.

5.Hayo magoli manne, kwa Waarabu ni dili,
Hiyo rekodi nyingine, mmewakata kauli,
Kwao huwa ni wengine, wanakuwa wakatili,
Mlivyotinga kibabe, hakika mmekomesha.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news