Mbunge Mpina asema kama alivyotumwa na Wanakisesa kuhusu hayati Ali Hassan Mwinyi


SALAAM ZA RAMBIRAMBI ZA WANANCHI WA JIMBO LA KISESA WILAYA YA MEATU KWA WATANZANIA NA FAMILIA YA MZEE ALI HASSAN MWINYI RAIS WA TANZANIA WA AWAMU YA PILI KWENYE IBADA MAALUM ILIYOFANYIKA KANISA LA WAADVENTISTA WASABATO MWANDOYA LEO TAREHE 2 MACHI 2024

Leo tarehe 2 Machi 2024 ni siku ya huzuni kwetu Watanzania wote siku ambayo Mzee wetu Alhaji Ali Hassan Mwinyi anazikwa huko Mangapwani Zanzibar baada ya kufariki tarehe 29 Februari 2024. 

Tunashukuru uongozi wa Kanisa la Waadventista Wasabato Mwandoya kwa kuandaa ibada maalum ya kuliombea Taifa, familia na watanzania wote katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wetu Rais wa Awamu ya Pili.

Wananchi wa Jimbo la Kisesa Wilaya ya Meatu wakiwemo wazee waliofanya kazi kwa karibu sana na Mzee Mwinyi, kwa pamoja tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huu wa kiongozi wetu, umetutia huzuni na simanzi kubwa kuondokewa na Mzee Wetu ambaye Taifa lilikuwa bado linategemea busara zake.

Tunamkumbuka Hayati Mzee Mwinyi kwa alama alizoacha na mchango mkubwa alioutoa kwa taifa letu akiwa Waziri, Balozi na baadaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kipindi cha uongozi wake tulishuhudia mageuzi makubwa ya Kisiasa na Kiuchumi ikiwemo kuruhusu mfumo wa Vyama vingi vya Siasa na kuruhusu Soko huria nchini.

Upande wa Wilaya yetu ya Meatu na Jimbo la Kisesa, tunamkumbuka Mzee Mwinyi kwa namna alivyotupenda wananchi wa Meatu kiasi cha kukubali maombi yetu yote yaliyopelekwa kwake na kupelekea kasi kubwa ya maendeleo wilayani kwetu na hapa tunaomba kutaja mambo matano kama ifuatavyo:-

(i) Hayati Mzee Mwinyi alikubali ombi la kuanzishwa kwa Wilaya mpya ya Meatu kutoka katika Wilaya ya Maswa, Wilaya ya Meatu ilianza rasmi mwaka 1987 baada ya Mhe. Rais Mwinyi kuridhia kuanzishwa kwake, Mzee Mwinyi akishirikiana na Viongozi wetu wa kipindi hicho akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Maswa kwa kipindi cha Mwaka 1975 hadi Mwaka 1980 na baadaye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Maswa na Mwenyekiti CCM Wilaya ya Meatu kati ya mwaka 1980 hadi 1995, Mzee Costantine Simenti Shilingi na viongozi wenzake wa wakati huo.

Tunakumbuka siku ya uzinduzi wa wilaya mpya ya Meatu Mzee Mwinyi alipofika Meatu alisema “Meatu mmetumia nguvu na rasilimali zenu nyingi kuijenga wilaya ya Maswa lakini leo mmeamua kujitenga na kuanzisha wilaya yenu hivyo wakati wenzenu Maswa wanatembea ninyi mnapaswa kukimbia” alisisitiza Mzee Mwinyi kuwa “itawabidi mkimbie wakati wenzenu wanatembea” maneno haya huwa hayatutoki moyoni na hapo ndipo harakati za kujiletea maendeleo katika wilaya yetu zikaanza kushika kasi kubwa.

(ii) Hayati Mzee Mwinyi aliridhia kuanzishwa Jimbo jipya la uchaguzi la Kisesa kutoka katika Jimbo la Meatu, Mzee Mwinyi baada ya kupelekewa maombi ya kugawa Jimbo la Meatu na Viongozi wetu akiwemo Mhe. Jeremiah Jisaba Mulyambate aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Meatu kipindi cha 1990 hadi 2005, Mzee Mwinyi alikubali na kuwezesha kuanzishwa Jimbo jipya la Kisesa na mwaka 1995 likafanya uchaguzi kwa mara ya kwanza.

Tangu hapo maendeleo ya Jimbo letu yakashika kasi kwa kuanzia na misingi aliyoiweka Mzee Mwinyi na wastaafu wenzake na leo tunashuhudia mageuzi makubwa ya maendeleo katika nyaja mbalimbali za elimu, afya, barabara, madaraja, umeme, maji, mawasiliano ya simu, kilimo, mifugo nk.

(iii) Hayati Mzee Mwinyi aliwezesha kujengwa kwa madaraja mawili makubwa ya Sanga Itinje na Minyanda kwenye barabara kuu ya Meatu-Shinyanga, kabla ya ujenzi wa madaraja hayo Meatu ilikuwa kisiwa na wananchi walikosa huduma muhimu za kijamii na Kiuchumi na hata watumishi wa umma walilazimika kukaa miezi 6 bila mshahara kutokana na mito kujaa maji na kushindwa kufika wilayani Maswa.

Tunakumbuka furaha na sherehe iliyofanyika katika uzinduzi wa madaraja hayo ambapo Rais Mwinyi alimtuma Waziri Mkuu wake wakati huo Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba kuja kuyazindua madaraja hayo.

(iv) Hayati Mzee Mwinyi alikomesha vita vya kikabila baina ya Wataturu, Wamasai na Wasukuma, kulikuwa na vita kubwa za kikabila zilizosababishwa na kushamiri kwa wizi wa mifugo ambapo Hayati Mzee Mwinyi aliimarisha ulinzi na mashirikiano baina ya kabila hizo na kufanikiwa kumaliza vita na ugomvi mpaka leo jamii hizi zinaishi kwa amani na mashirikiano makubwa.

(v) Hayati Mzee Mwinyi alisaidia kupatikana kwa bei nzuri ya zao la Pamba, katika Sera zake za kuruhusu soko huria ambako kulichochea ushindani na kuwezesha kupatikana kwa bei nzuri ya zao la Pamba na mazao mengine katika Jimbo letu na sehemu nyingine nchini na kuwezesha wananchi wengi kunufaika na kilimo ikiwemo kujenga nyumba bora za kuishi.

Hayati Mhe. Alhaji Ali Hassan Mwinyi ataendelea kuwa kielelezo cha uongozi bora katika taifa letu hasa alipokubali kuwajibika na kujiuzulu wadhifa wake wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa makosa yaliyofanywa na wengine. Dhana hii ya Uwajibikaji ni nadra sana kupatikana kwa Viongozi, Mzee Mwinyi ataendelea kuwa darasa la uongozi kwa kizazi cha sasa na kijacho.

HITIMISHO

Tutaendelea kumkumbuka na kuenzi kazi na Wema wake usiomithilika kwa Taifa letu la Tanzania na Wilaya yetu ya Meatu, tunajua hapa Duniani kuna makazi ya wafu na makazi ya walio hai lakini mapenzi yetu kwake hayawezi kutenganishwa na kifo, tutaendelea kukukumbuka na kukuombea daima.

Pia tunaendelea kutoa pole nyingi kwa Watanzania wote, familia na kwa Dk. Hussein Ali Mwinyi (Mtoto wa Marehemu) na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Salamu za pole pia kwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuondokewa na hazina ya ushauri na nguzo muhimu katika uongozi na ujenzi wa Taifa letu. 

Tunaamini Mwenyezi Mungu hatatuacha katika kipindi hiki kigumu ataendelea kutujaza faraja na matumaini. Mungu hataiacha familia ya Hayati Mzee Mwinyi, Mungu wa wanyonge, Mungu wa Yatima, Mungu wa Wajane hatawaacha kamwe.

Kutokana na msiba wa Mzee Mwinyi, Wazee wa Jimbo la Kisesa walikutana tarehe 1 Machi 2024 kujadili namna ya kushiriki maziko ya kiongozi wao ambapo waliandaa salamu za rambirambi na kuchanga Ng’ombe 2, Mbuzi 10 na Fedha taslimu Tsh. Milioni 1 kama sehemu yao ya kushiriki msiba huo. 

Pia wakakubaliana kuteua wazee wawili na Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina kwenda visiwani Zanzibar kuhani msiba na kukabidhi rambirambi hizo kwa familia ya Hayati Ali Hassan Mwinyi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kisesa.

Mwisho

Tunalishukuru sana Kanisa la Waadventista Wasabato Mtaa wa Mwandoya Conference ya SNC wakiongozwa na Mchungaji Faustine Magashi kwa kukubali ombi la wazee wa Jimbo la Kisesa kuendesha ibada maalum ya kuliombea Taifa, Watanzania na Familia ya Mzee Ali Hassan Mwinyi kufuatia kifo cha Kiongozi huyo mashuhuri.

Bwana alitoa na Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe Amen.

Salaam hizi zimesomwa na Mhe. Luhaga Joelson Mpina Mbunge wa Jimbo la Kisesa kwa niaba ya wananchi na wazee wa Jimbo la Kisesa tarehe 2 Machi,2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news