Mtoto aliyekutwa na tatizo la kumeza chakula afanyiwa upasuaji matundu madogo kuondoa zuio Muhimbili

DAR ES SALAAM-Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imemfanyia upasuaji kwa njia ya matundu madogo (Laparoscopic Hellers Myotomy) mtoto wa miaka saba ambaye alikua na tatizo la kumeza.

Ni tatizo linalojulikana kwa kitaalam kama Achalasia Cardia tangu akiwa na umri wa mwaka moja kutokana na mishipa yake ya fahamu ya koo la chakula kuharibika na kumfanya ashindwe kumeza kwa urahisi.
Daktari Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Mfumo wa Chakula, Ini na Mbobezi wa Upasuaji wa Matundu Madogo, Dkt. Kitembo Kibwana ambaye ameongoza jopo la watalaam wenzake amesema, upasuaji huo ulifanyika ili kupunguza kizuizi kati ya umio (koo la chakula) na tumbo.

Sambamba na kugawanya safu ya misuli kutoka kwenye umio hadi tumbo ili kumuwezesha mtoto huyo kumeza chakula kwa urahisi.

Dkt. Kibwana amesema, Achalasia ni ugonjwa ambao hufanya iwe vigumu kwa chakula na kioevu kupita kutoka koo la kumeza linalounganisha kinywa na tumbo (umio) ndani ya tumbo na kuongeza kuwa tatizo.

Amesema,hili hutokana na mishipa kwenye umio kuharibiwa na mwili wenyewe (auto-immune) au baadhi ya maambukizi na kusabaisha umio kupooza na kupanuka kwa muda na hatimaye kupoteza uwezo wa kukamua chakula hadi tumboni.

Daktari huyo amesema, matokeo yake chakula hicho hujikusanya kwenye umio, wakati mwingine huchacha na kurudishwa hadi mdomoni kikiwa na ladha chungu.

Amewataka wananchi wenye changamoto ya kumeza (Achalasia) kufika hospitali ili kufanyiwa uchunguzi na kisha kupatiwa matibabu stahiki,kwani huduma hiyo hutolewa kwa muda mfupi na kumruhusu mgonjwa ndani ya siku angalau mbili kwenda nyumbani kuendelea na shughuli zake.

“Mpaka sasa tumeweza kufanya upasuaji wa aina hii kupitia njia ya matundu (Laparoscopy) kwa wagonjwa wapatao 24 kwa ufanisi mkubwa zaidi ambapo kati ya hai, 3 ni watoto,” ameeleza Dkt. Kibwana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news