PIC yawapa heko NHC, yaahidi kuishawishi Serikali itoe fedha

DAR ES SALAAM-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imesema kuwa, itaishawishi Serikali itoe fedha kwa wakati ili Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) liweze kukamilisha miradi yake kwa wakati iweze kuleta tija kwa Serikali na Taifa kwa ujumla.
Pia,PIC imelipongeza shirika hilo kwa kutekeleza miradi mikubwa mitatu iliyopo jijini Dar es Salaam kwa ufanisi wa hali ya juu.

Akizungumza mara baada ya kamati hiyo kutembelea miradi hiyo leo Machi 20,2024 jijini Dar es Salaam,Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deus Sangu amesema kuwa, katika kikao kijacho cha Bunge la Bajeti wataendelea kuishawishi Serikali kutoa fedha ili NHC iweze kukamilisha miradi hiyo.
"Tumetembelea miradi ya 7/11 Kawe, Morocco Square na mradi wa Samia House Scheme kwa kweli tumejionea ni miradi mikubwa ambayo ikikamilika italeta mrejesho mzuri kwa Serikali.

"Hivyo basi, kama Kamati katika kikao cha Bunge la Bajeti lijalo tutaendelea kuishawishi Serikali itoe fedha ili miradi hiyo ikamilike.
"Mfano tumeona mradi wa Kawe nyumba zote zimekwishachukuliwa, mradi wa Morocco pia vivyo hivyo na baada ya kukamilika tu tunatarajia mrejesho mzuri sana na faida kwa serikali,"amesema.

Mwenyekiti huyo ametoa rai kwa Serikali kutoa fursa kwa kuruhusu watanzania waishio nje ya nchi na wageni kushiriki katika kuwekeza kwenye sekta ya uendelezaji miliki.
Amesema kuwa, wataendelea kuishawishi Serikali kwa kuieleza faida ya uwekezaji kwa wageni na watanzania waishio nje ya nchi katika miradi ya shirika hilo la nyumba.

Vile vile, amempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa vibali kwa shirika hilo ili liweze kukopa na kufanya miradi ya uwekezaji.

Amesema kuwa, kutokana na uwekezaji mkubwa kwenye miradi hiyo mitatu rejesho la faida kwenye miradi hiyo inaendelea kuonekana ndani ya muda mchache.

Kamati hiyo imetembelea mradi wa Morocco Square, Mradi wa 7/11 na Samia Housing Scheme yote ikwa jijini Dar es Salaam.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah Hamad ameishukuru kamati hiyo kwa ushauri ambao wamekuwa wakiutoa ndani na nje ya Bunge.

Amesema, ili sekta ya nyumba iweze kustawi vizuri wanaendelea kuishawishi serikali kufanya sekta ya nyumba kuwa kipaumbele cha Taifa, Serikali kuondoa vikwazo vyote vinavyozuia watanzania waishio ughaibuni pamoja na raia wa mataifa mengine kushiriki katika kuwekeza kwenye sekta ya uendelezaji miliki.

Pia kuwe na sera inayoleta unafuu wa kodi kwenye vifaa vya ujenzi na ongezeko la thamani kwenye nyumba za gharama nafuu pamoja na serikali kuanzisha mfuko maalum wa kusaidia ruzuku kwenye nyumba za gharama nafuu.
Mkurugenzi huyo ameahidi kufanya kazi kwa weledi ili kuleta tija kwa serikali na Taifa kwa ujumla na kwamba kwenye miradi hiyo kwa upande wa nyumba za makazi tayari nyumba 60 kati ya 100 zimekwishauzwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news