Serikali kujenga maabara ya kisasa ya upimaji wa sampuli za madini nchini

DODOMA-Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluh Hassan imejipanga katika mwaka wa Fedha 2024/25 kuanza ujenzi wa maabara kubwa na ya kisasa na yenye vifaa vya kisasa ya upimaji sampuli za madini itakayojengwa katika eneo la Kizota jijini Dodoma ili kuendana na kasi ya ukuaji wa Sekta ya Madini nchini na matarajio ya wadau kwa ujumla.
Ujenzi huo wa maabara kubwa na ya kisasa utakwenda sambamba na ujenzi wa maabara za kanda na kuwajengea uwezo watumishi wa GST ili kuendana na kasi kubwa ya maendeleo ya Teknolojia duniani.

Mhe. Mavunde aliyasema hayo jana Aprili 24, 2024 jijini Dodoma katika kikao cha pamoja cha kujadili namna bora ya utendaji kazi kilichowakutanisha Watumishi wote wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).“Jukumu letu la kimsingi ni kuhakikisha kwamba taasisi hii inatoa mchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya madini hapa nchini Tanzania."

Aliongeza kwamba, taarifa za maabara kutoka GST zinapaswa kuwa za uhakika na sahihi kwa wachimbaji jukumu ambalo kama ambalo kama serikali haliwezi kulikwepa.

"Tumedhamiria kuhakikisha tunajenga maabara kubwa, ya kisasa na tegemeo katika utoaji wa huduma ndani na nje ya mipaka Tanzania,"alisema Mavunde.
Pia, Waziri Mavunde aliongeza kuwa GST ina mchango mkubwa katika ukuaji wa Sekta ya Madini huku akisisitiza kwamba GST ni Moyo wa Sekta ya Madini nchini, kutokana na umuhimu huo Serikali imeendelea kuiwezesha zaidi GST ili itekeleze majukumu yake kwa ufanisi unaotarajiwa.

Mavunde alitumia fursa hiyo kuwataka watumishi wote kujituma na kufanya kazi kwa weledi katika kutekeleza majukumu ya GST na kusisitiza kwamba hatakuwa tayari kumvumilia mtu yoyote ambaye hatakuwa tayari kuchapa kazi kwa bidii ili kufikia maono na matarajio ya Wizara na wadau kwa ujumla.

Pia, alisema umoja na mshikamano ndiyo kitaisaidia taasisi hiyo kusonga mbele na kuwataka watumishi wote kufanya kazi kama timu moja na kuongeza, "kwa umoja wetu utasaidia kufikia malengo tuliyojiwekea ya kufanya utafiti wa kina wa asilimia angalau 50 ifikapo mwaka 2030.
Akitoa maelezo ya awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Kheri Abdul Mahimbali aliwaahidi watumishi wa GST kushughulikia changamoto mbalimbali za kiutumishi walizonazo ili kuboresha mazingira yao ya kufanya kazi.Akitoa salamu za shukrani, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba aliishukuru Serikali kwa kuipa kipaumbele Taasisi ya GST na kuahidi kusimamia utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa ili kuongeza na kuboresha ufanisi wa taasisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news