Serikali ya wanafunzi OUT yapongezwa kwa utendaji kazi bora

KIGOMA-Menejimenti ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) imeipongeza serikali ya wanafunzi wa OUT kwa utendaji kazi wake bora na ushirikiano wake wa karibu na uongozi wa chuo, unaofanya mambo magumu kwa wanafunzi kuwa mepesi na yenye kutatulika.
Hayo yamedhihiri Aprili 18, 2024 wakati wa mkutano wa 43 wa baraza la wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania unaofanyika katika kampasi ya chuo hiki iliyopo Ujiji katika Manispaa ya Kigoma ambapo Makamu mkuu wa chuo hiki Prof. Elifas Bisanda amefungua rasmi mkutano wa baraza hilo.

Katika ufunguzi huo Prof. Bisanda amesema, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinathamini jitihada zinazofanywa na serikali ya wanafunzi katika kuboresha na kutatua changamoto za wanafunzi kwa kushirikiana bega kwa bega na menejimenti ya chuo katika kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa wanafunzi.

Akiongeza, ameisihi serikali hiyo kuendelea kushirikiana na menejimenti hususani viongozi wapya ambao wameteuliwa kushika ngazi mbalimbali za kitaasisi ikiwemo ngazi ya menejimenti, Wakurugenzi na wakuu wa vitengo na idara ikiwa ni mabadiliko makubwa kutokana na viongozi wake wengi kumaliza muda wao na wengine kupata teuzi mbalimbali serikalini zinazowafanya kuwa nje ya taasisi na hivyo kuhitaji mbadala wake.
“Mkuu wa Chuo, Mhe. Mizengo Kayanza Pinda, amemteua Prof. Alex Makulilo kuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Tafiti na Ushauri wa Kitaalamu ambaye anachukua nafasi ya Prof. Deus Ngaruko anayemaliza muda wake. Wakati huo huo amemteua Prof. Josiah Katani kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), kuhudumu nafasi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Fedha, Mipango na Utawala akichukua nafasi ya Prof. George Oreku ambaye amemaliza muda wake,” amesema Prof Bisanda.

Ameendelea kusema baraza la chuo limeteua wakurugenzi kadhaa kushika nafasi za ukurugenzi na Menejimenti ya chuo imeteua wakuu wa vitengo na idara mbalimbali za chuo kwa lengo la kuendeleza utendaji kazi mzuri uliofanywa na viongozi waliomaliza muda wao.

Pia ameongeza kwamba, kupitia mradi wa Mageuzi ya Elimu ya Juu kwa mabadiliko ya kiuchumi (HEET) chuo kinajenga maabara za masomo na fani za sayansi katika kanda saba nchini, kimepeleka wahadhiri 25 kwenye masomo ya shahada za umahiri na uzamivu ndani na nje ya nchi na kinapitia upya mitaala yake. Pia, kinaendeleza wasichana kwenye masomo ya sayansi kupitia foundation program na kujenga kituo cha utafiti Kibaha mkoani Pwani. Hii yote ni kwa ajili ya kuimarisha huduma za ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Akiongea katika mkutano huo Rais wa Baraza la Wanafunzi wa chuo hiki, Ndg. Felix Lawrence Lugeiyamu, amesema ushirikiano wa karibu uliopo baina ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Baraza la wanafunzi unafanya wanafunzi wa chuo hiki kujisikia wapo karibu zaidi na chuo chao katika nyakati zote za masomo yao.

“Utendaji kutoka kwa menejimenti na wafanyakazi wa chuo umekuwa ni rafiki sana hata hoja iwe ngumu vipi itatafutiwa ufumbuzi, kutokana na ushirikiano huu Makamu Mkuu wa chuo hatukualiki hapa kukupatia malalamiko yetu bali tumekualika tuweze kukusikiliza kwa sababu hatusubiri vikao kuwasilisha changamoto bali huziwasilisha pale zinapotokea na ufumbuzi hupatikana mara moja,”amesema Ndg. Lugeiyamu.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kumuaga Naibu Makamu Mkuu wa chuo, Taaluma, Tafiti na Ushauri wa Kitaalamu anayemaliza muda wake, Prof. Deus Ngaruko na kumshukuru kwa kuwa ni miongozi mwa viongozi walioshiriki katika kukiletea chuo hiki maendeleo makubwa katika kipindi chake cha miaka 8 ya uongozi katika wadhifa huo.

"Prof. Ngaruko amekuwa akipatikana muda wote bila kujali kikwazo cha muda na atafanyia kazi hoja husika kwa wakati na kutoa mrejesho. Hii ni sifa yake kuu na ndio maana leo tunampongeza kwa utendaji uliotukuka ulioleta ufanisi na tija katika chuo chetu,"amesema Ndg. Lugeiyamu.

Naye Prof. Deus Ngaruko, akizungumza katika baraza hilo kwa mara ya mwisho akiwa kama Naibu Makamu Mkuu wa chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri wa Kitaalamu amewataka viongozi wa wanafunzi kuendeleza ushirikano wa karibu na menejimenti kwani ukaribu huo umeifanya kazi yake kuwa nyepesi. Amesema nafasi hiyo ndiyo inayogusa moja kwa moja mahitaji muhimu ya wanafunzi chuoni. Kupitia ukaribu huo hakupata changamoto na wanafunzi na lilipojitokeza tatizo lilitatuliwa mapema kabisa ya bila kuzua taharuki ya aina yoyote.
Mkutano wa 43 wa Baraza la Wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania unafanyika kwa siku nne kuanzia Aprili 17 hadi Aprili 20 katika kampasi ya chuo kituo cha mkoa wa Kigoma iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo wawakilishi wa wanafunzi wa chuo hiki kila mkoa wanashiriki katika kujadili mambo mbalimbali yenye lengo la kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika kuimarisha zaidi huduma kwa wanafunzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news