Serikali yaahidi mshikamano zaidi kwa shule binafsi nchini

DAR ES SALAAM-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi hususan shule binafsi ili kuboresha sekta ya elimu nchini.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi Nchini (TAPIE), leo Aprili 27, 2024 jijini Dar es salaam Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan haiwezi kuacha Wadau wa Elimu wakilalamika, kwa kuwa uwepo wao unaisaidia Serikali.
“Nataka niwahakikishie kuwa Serikali imeendelea kukutana na TAPIE mara kwa mara, na hapa namuelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama kuratibu mkutano wa pamoja kati ya TAPIE na Wizara za Ardhi, Fedha, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kujadiliana kwa pamoja na kupata suhulu ya changamoto zinazowakabili”, amesema Dkt. Biteko.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa TAPIE kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika barua na vyeti vya usajili wa asasi zao, kwa kuwa kuna baadhi hukiuka masharti hivyo kusababisha migongano isiyo ya lazima na mamlaka zilizokasimiwa kusimamia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya uendeshaji wa asasi za elimu nchini.

Vilevile, amewataka kufuata sheria na kanuni za utoaji elimu, kuhimiza na kuimarisha maadili, nidhamu na malezi bora kwa watumishi na wanafunzi walio chini ya asasi zao. Pia, amesema kuwa suala la uadilifu katika shughuli za uendeshaji na usimamizi wa mitihani ya Kitaifa lisisitizwe na kutiliwa mkazo ili kupata wataalam wenye sifa stahiki.
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amezipongeza shule binafsi kwa kufanya uwekezaji mkubwa ambao sasa unavutia baadhi wanafunzi kutoka nchi zingine kuja kusoma hapa nchini

“Tunapozungumza kuwa tunaenda na elimu ya miaka 10 tunaamini sekta binafsi ina msaada mkubwa katika hili kwa sasa tutanza na ujenzi wa shule 100 za sekondari za ufundi na ni imani yangu kuwa tutashirikiana vizuri na sekta binafsi”, amesisitiza Prof. Mkenda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Husna Sekiboko amesema kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi katika sekta binafsi na sasa kuna zaidi ya shule 500. Pia, amempongeza Rais Mhe. Dkt. Samia kwa kutoa maelekezo ya kuboresha sekta ya elimu nchini.
“Tunaipongeza sekta binafsi kwa kutoa ajira na Bunge tunatambua mchango wa TAPIE, tutawaunga mkono katika kuboresha sekta hii ya elimu. Kuhusu leseni ya kuanzisha shule, Kamati yangu inaungana na TAPIE tunaoomba Serikali izungumze na wadau ili kusaidia kupiga hatua ya utekelezaji wa mitaala iliyowekwa,”ameeleza Mhe. Sekiboko.

Sambamba na hayo, ameitaka TAPIE kulinda mikataba ya watumishi walio chini ya Taasisi zao ikiwa ni pamoja na kuwasilisha michango yao katika Mifuko ya Hifadhi za Jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news