Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) yaachia mkeka wa nguvu washiriki Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu itakayofanyika Jumamosi hii

DAR ES SALAAM-Mshindi wa Tuzo ya Nobel ya mwaka 2021 katika fasihi, Prof. Abdulrazak Gurnah, anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania kwa mwaliko wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda. 

Prof Gurnah ndiye mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu itayofanyika Aprili 13, 2024 katika ukumbi wa The Super Dome Masaki Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) inayoratibu utoaji wa tuzo hiyo, Dkt. Aneth Komba amesema kuwa, Profesa Gurnah atapokelewa na viongozi mbalimbali katika Uwanja wa Ndenge wa Kimataifa wa Julius Nyerere siku ya Ijumaa ya tarehe 12 Aprili 2024 akitokea nchini Uingereza.

"Moja ya malengo ya tuzo hii ni kumuenzi baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika kazi kubwa aliyoifanya kwenye eneo la uandishi,"amesema Dkt.Komba.

Ameongeza kuwa, kabla ya hafla ya tuzo hiyo, Prof.Gurnah atapata nafasi ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na waandishi bunifu nchini kwa lengo la kubadilishana nao mawazo mbalimbali kuhusu uandishi bunifu.
Pia amesema kwamba, wageni wengine katika hafla hiyo ni waandishi maarufu kutoka nchi za Kenya na Uganda ambao wataungana na waandishi bunifu wa Tanzania katika hafla ya tuzo hiyo na watapata nafasi ya kutoa uzoeafu wao katika eneo la uandishi bunifu.

Prof. Gurnah ni mwandishi wa fasihi na alikuwa mshindi katika Tuzo ya Nobel ya mwaka 2021 iliyofanyika nchini Sweden.

Tuzo hiyo ya Taifa inajumuisha vipengele vya Riwaya, Ushairi na Hadithi za Watoto ambapo washindi wa kwanza katika vipingele hivyo watapata zawadi ya shilingi milioni kumi kila mmoja.
Tuzo hiyo inafanyika nchini kwa mara ya pili sasa ambapo kwa mara ya kwanza ilifanyika mwaka 2023 .

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news