TARURA:Mabey Bridge kuunganisha Kata ya Mbingu na Namwawala wilayani Kilombero

MOROGORO-Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA imekamilisha ujenzi wa Daraja la Chuma la mto Lwipa (Mabey Bridge) lenye urefu wa mita 27 na matengenezo ya barabara ya Kisegese – Chiwachiwa – Lavena yenye urefu wa Km 15 kwa gharama za shilingi bilioni 1.8.
Kukamilika kwa daraja hilo limewezesha kuunganisha Kata ya Mbingu na Namwawala katika Halmashauri ya Mlimba, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilombero Mhandisi Sadiki Kalumi amesema ujenzi wa Daraja hilo lililojengwa na wataalam kutoka TARURA litarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji katika maeneo hayo.
“Daraja hili lina urefu wa mita 27 limegharimu shilingi milioni 900, lakini pamoja na Daraja kuna matengenezo ya Barabara ambayo itajengwa kwa kiwango cha changarawe pamoja na makalavati kwa gharama ya shilingi milioni 900 kufanya jumla ya shilingi Bilioni 1.8."

Mhandisi Sadiki amesema hapo awali wananchi walikuwa wakitumia gogo kuvuka kabla ya kujengwa kwa Daraja la mbao ambalo lilikuwa si la uhakika kabla ya TARURA kujenga Daraja la Chuma katika Mto huo na kuchochea shughuli za Kilimo katika maeneo hayo ya Chiwachiwa na Kisegese.

“Wakazi wa maeneo haya wanajishughulisha na Kilimo cha Kokoa, Mpunga, Mahindi, Mawese, Ufuta pamoja na Ndizi hivyo daraja hili ni mkombozi kwani litawaletea maendeleo na kuwainua kiuchumi”.
Pia, Meneja huyo amewataka wanachi hao kuwa walinzi wa daraja hilo.

Naye, Diwani wa Kata ya Mbingu Mhe. Nestory Kelula amesema wakazi wa Kata ya Mbingu ambao ni wakulima walipata tabu katika kusafirisha mazao yao kutoka Chiwachiwa hadi Kisegese kwa kuwa kulikuwa hakuna mawasiliano hivyo kuwalazimu kusafirisha mazao kwa kutumia baisikeli kwa gharama kubwa na kushindwa kuona thamani ya mazao yao.

“Kukamilika kwa Daraja la Mto Lwipa wakulima wa Mbingu watanufaika na mazao yao.Kwakweli tunamshukuru Mhe. Rais kwa namna ambavyo ametusaidia wananchi wa vijiji hivi”.
Naye Bw. Raymond Samson Mkazi wa Kijiji cha Kisegese anasema,kukamilika kwa Daraja hilo litawasaidia katika usafirishaji wa mazao yao katika vipindi vyote vya mwaka kwani walikuwa wanapata tabu kutokana na uwepo wa Daraja la mbao kushindwa kupitika hasa katika kipindi cha mvua.

TARURA inaendelea na utatuzi wa changamoto za miundombinu katika maeneo mbalimbali hasa katika kipindi hiki cha mvua ili kuhakikisha mawasiliano yanarejea katika maeneo yote yaliyoathirika pamoja na ujenzi na matengenezo ya barabara pamoja na vivuko.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news