Zinabaki kazi zake,Kwaheri Zephania Ubwani

NA LWAGA MWAMBANDE

ZEPHANIA Ubwani ambaye ni mwandishi mkongwe nchini amefariki.
Mzee Ubwani ambaye alikuwa anahudumu katika Gazeti la Citizen jijini Arusha amefariki leo Aprili 6,2024 wakati akiendelea kutekeleza majukumu yake ya kila siku ya kihabari.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na mtandao wa Mwananchi ambao umefafanua kuwa, Mzee Ubwani amefikwa na umauti ghafla.

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande amesisitiza kwamba, kuondoka kwa mzee Ubwani ni pigo kwa tasnia ya habari ingawa zinabaki kazi zake. Endelea.

1.Alijua kazi yake, alitunza hadhi yake,
Kwa kweli nafasi yake, ametuacha wapweke,
Huyo kaondoka zake, imefika zamu yake,
Ni Zephania Ubwani, zinabaki kazi zake.

2.Kufika habari yake, ya kwamba kaenda zake,
Yaja kumbukumbu yake, hata ule mwendo wake,
Na pia mavazi yake, utambulisho wa kwake,
Ni Zephania Ubwani, zinabaki kazi zake.

3.Ile kalamu ya kwake, na nyingi habari zake,
Kutokea enzi zake, kwa sisi wadogo zake,
Na hata uzee wake, alishika kazi yake,
Ni Zephania Ubwani, zinabaki kazi zake.

4.Ule utendaji wake, na kuaminika kwake,
Alijenga jina lake, levo yake peke yake,
Kweli twajifunza kwake, kwa ile heshima yake,
Ni Zephania Ubwani, zinabaki kazi zake.

5.Ni nyingi habari zake, na hata makala zake,
Kingereza lugha yake, tafuta habari zake,
Mbali sana mwanzo wake, sasa ndiyo mwisho wake,
Ni Zephania Ubwani, zinabaki kazi zake.

6.Kwa ile nafasi yake, uandishi kazi yake,
Lipata heshima yake, kwa wadogo na wenzake,
Ule msimamo wake, wa kujali kazi yake,
Ni Zephania Ubwani, zinabaki kazi zake.

7.Jumuiya hii yake, kwa zile habari zake,
Ni tokea enzi zake, kutokea iinuke,
Kwa kweli mchango wake, alifanya kazi yake,
Ni Zephania Ubwani, zinabaki kazi zake.

8.Mahakama ile yake, ya kimbari kazi zake,
Kwa lile jukumu lake, lifanya ieleweke,
Na hadi mwisho ifike, wengine watawanyike,
Ni Zephania Ubwani, zinabaki kazi zake.

9.Maarufu jina lake, sawasawa kazi zake,
Ni nani nafasi yake, Arusha pale ashike,
Hivi nani ainuke, hadhi yak wake afike?
Ni Zephania Ubwani, zinabaki kazi zake.

10.Kamaliza kazi yake, twaziimba sifa zake,
Kaondoka peke yake, ghalfa tena kivyake,
Kila mtu zamu yake, Rabuka mipango yake,
Ni Zephania Ubwani, zinabaki kazi zake.

11.Pole familia yake, ndugu marafiki zake,
Pia tasnia yake, kwa ule mchango wake,
Mema ya kwake tushike, na wala yasifutike,
Ni Zephania Ubwani, zinabaki kazi zake.

12.Pole na kwa vyombo vyake, akofanya kazi zake,
Mwajua mchango wake, ombwe kuondoka kwake,
Endelea msichoke, waibue waibuke,
Ni Zephania Ubwani, zinabaki kazi zake.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news