Elimisheni jamii juu ya OUT na huduma zake-Dkt.Hellar-Kihampa

TANGA-Wito umetolewa kwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT) kutumia fursa ya Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu kutoa elimu kwa wadau mbalimbali watakaotembelea banda la chuo hiki katika maadhimisho hayo pamoja na kuonesha bunifu na ujuzi katika tafiti mbalimbali ili kuiwezesha jamii kukifahamu vizuri Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na huduma zake.Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Taaluma za Awali, Dkt. Harieth Hellar-Kihampa, alipotembelea banda la chuo hiki jijini Tanga katika Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu akimuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania,Prof. Elifas Bisanda.

Amewataka watumishi wa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania wanaotoa huduma ya uelimishaji kwenye maonesho haya wawe wabunifu na wawe na utayari kuhudumia wageni ili kuzidi kukisogeza chuo kwa jamii na kiweze kufahamika zaidi kwa wanafunzi wanaotarajia kuanza kujiunga na vyuo hivi karibuni.
“Napenda kuwapongeza Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania kwa maandalizi mazuri na kuifanya taasisi yetu kushiriki kikamililifu katika Maadhimisho haya.

"Banda letu limejizatiti vizuri, huduma za ubunifu nimeona zipo nyingi, programu za chuo ngazi zote, huduma kwa watu wenye mahitaji maalumu na tafiti zilizofanywa na wanataaluma wa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania zipo tayari kuoneshwa kwa Umma.

"Haya ni mafanikio makubwa, natarajia wananchi watafurahia huduma na kujifunza mambo mengi mazuri kutoka Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania,” amesema Dkt. Hellar-Kihampa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akifungua maadhimisho hayo amehimiza Watanzania kutembelea maadhimisho hayo kujionea maendeleo na mageuzi yanayofanyika katika sekta ya elimu nchini.

Aidha ameziasa taasisi za elimu ya juu kutembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika maadhimisho hayo kwa lengo la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kupeana mikakati ya kusukuma mbele maendeleo ya taifa letu.
Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yameshirikisha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yanaendelea kurindima katika viwanja vya shule ya sekondari Popatlal tangu Mei 25 na yanatarajiwa kufika tamati Mei 31, 2024 jijini Tanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news