Simba SC yavuna alama tatu kwa KMC FC

ARUSHA-Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam imevuna alama tatu kutoka kwa majirani zao KMC FC ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam baada ya kuwachapa bao moja.
Ni baada ya wageni hao kumenyana Mei 25,2024 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ikiwa ni mwendelezo wa michezo ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Kupitia mchezo huo ambao ulionekana mkali na kuvutia muda wote, bao pekee la Simba SC limefungwa na Saido Ntibazonkiza dakika ya tatu baada ya kumzidi ujanja mlinda mlango wa KMC, Denis Richard.

Aidha, baada ya bao hilo mchezo uliendelea kuwa wa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu, lakini hakukuwa na ufanisi katika eneo la mwisho.

Kipindi cha pili timu zote zilirudi kwa kasi huku mpira ukichezwa zaidi eneo la katikati ya uwanja.

Kocha Juma Mgunda alifanya mabadiliko ya kuwatoa Willy Onana, Ladaki Chasambi na Ntibazonkiza na kuwaingiza Edwin Balua, Luis Miqussone na Saleh Karabaka.

Ushindi huo unawafanya Simba kufikisha pointi 66 wakiendelea kusalia nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi.

Aidha, KMC kwa wao baada ya kupoteza mchezo wa huo wanabaki na alama zao 39 nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news