Tanzania kushika Ukurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)

NAIROBI-Tanzania inatarajia kushika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji mbadala (Alternative Executive Director) katika Kundi la Magavana wa Afrika Mashariki katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kuanzia mwezi Agosti, 2024.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba ameyasema hayo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati wa Mkutano wa kawaida wa Magavana wa Kundi la Nchi za Afrika Mashariki ambao ni wanachama wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ikiwa ni maandalizi ya Mikutano ya Mwaka 2024 ya Bodi ya Magavana (Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama) wa Benki hiyo inayofanyika jijini Nairobi nchini Kenya.
Dkt. Mwamba alieleza kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika imeweka utaratibu wa mzunguko wa uongozi katika Nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki ambao ni Mkurugenzi Mtendaji na Mshauri na kwa upande wa Tanzania kunakuwa na Mkurugenzi Mtendaji mbadala (Alternative Executive Director).

‘’Katika mkutano huu tumezungumzia pia mzunguko wa viongozi ambao ni Mkurugenzi Mtendaji na Mshauri na sisi Tanzania kuanzia mwezi Agosti, 2024 tutashika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji Mbadala katika Benki hiyo ambaye atakuwa anachukua nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji anapokuwa anapata udhuru,’’ alisema Dkt. Mwamba.
Aidha, Dkt. Mwamba alisema kuwa mkutano huo ulijadili kuhusu mabadiliko ya tabia nchi ambayo hivi karibuni yamekuwa yakisababisha maafa mbalimbali na kukubaliana kuanzishwa kwa mfuko wa maafa ambao utakuwa unasaidia nchi zitakazo athirika na mabadiliko hayo ikiwemo mvua zisizotarajiwa za El nino.

“Tumejadili pia kuhusu mabadiliko ya tabianchi na namna ya kuongeza mtaji lakini pia nchi zilizopata majanga ya mafuriko yaliyosababishwa na mvua nyingi zilizojitokeza mwaka huu pia itakuwa ajenda itakayojadiliwa katika Mkutano Mkuu,”aliongeza Dkt. Mwamba.
Mkutano wa Kundi la Nchi za Afrika Mashariki ambao umeshirikisha Wajumbe kutoka nchi tisa (9) ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia, Somalia, South Sudan, Eritrea na Seychelles, ni utangulizi wa Mkutano wa 59 wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika Nairobi, Kenya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news