BERLIN-Ujerumani ni miongoni mwa mataifa yaliyopiga hatua kubwa katika maendeleo hasa kwenye sekta ya elimu hususani matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ufundishaji na ujifunzaji.

Kiongozi wa ujumbe huo, Prof. Alex Makulilo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu akiwa katika ziara hiyo kwenye Chuo Kikuu cha Bremen amesema ziara hii imekuwa ni ya muhimu sana hasa ukizingatia ukuaji wa matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na kujifunza kwa wenzetu.

"OUT ni wadau muhimu katika kutumia mifumo hii kwa ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi wetu, tunaamini tunayojifunza hapa yatatusaidia kuimarisha zaidi mifumo yetu na kuendelea kutoa elimu bora kwa wanafunzi wetu," amesema Prof. Makulilo.
Ameongeza kuwa, ziara hii ni zao za ushirikiano uliopo baina ya OUT na Chuo Kikuu cha Bremen, kupitia mashirikiano hayo taasisi hizi mbili hubadilishana uzoefu na kuimarishana zaidi katika maeneo ya ufundishaji, ujifunzaji, utafiti na Ushauri wa Kitaalamu kwa jamii zao. Eneo la kuwafanyia tathimini wanafunzi kupitia mifumo ya TEHAMA ni eneo nyeti ambalo linahitaji umakini mkubwa na OUT tumekuwa tukijifunza kupitia wenzetu ili nasi tuendelee kubuni mifumo bora zaidi katika eneo hili.
Wanataaluma wengine walioambatana katika ziara hiyo ni pamoja na Prof. Matobola Mihale ambaye ni Mtiva wa Kitivo cha Sayansi, Teknolojia na Taaluma za Mazingira, Dkt. Harrieth Mtae Mkurugenzi wa Utafiti, machapisho na ubunifu, Dkt. Thimoth Lyanga mratibu msaidizi wa mradi wa HEET wa OUT na Dkt. Halima Kilungu ambaye ni Mkuu wa Idara ya Jografia, Utalii na Ukarimu ya OUT ambao kwa pamoja wanakiri kwamba ziara hii ni muhimu sana katika kupata uzoefu wa wenzetu katika matumizi ya TEHAMA katika kutoa elimu.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wengine Dkt. Harrieth Mtae anasema ni jambo la kuishukuru Menejimenti ya OUT kuwezesha ziara hiyo katika Chuo Kikuu cha Bremen nchini Ujerumani kwani wenzetu wamepiga hatua kubwa kwenye mambo mbalimbali ikiwemo matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji.
“Tumechota mengi ambayo tutayatumia kujiimarisha zaidi kutoa taaluma bora kwa wanafunzi kupitia kuimarisha mitaala, kuandaa zana za kufundishia na kujifunzia na kufanya tafiti kwa manufaa ya nchi yetu," amesema Dkt. Mtae.
