Waziri Mkuu afurahishwa na mafunzo ya TEHAMA kwa watu wenye ulemavu

DODOMA-Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, ameonesha kufurahishwa na Mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanayotolewa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Majaliwa, ameonesha furaha hiyo katika Maonesho ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari alipotembelea banda la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wanaoshirikiana na Tume ya TEHAMA nchini katika maonesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma, kuanzia Mei 16 hadi Mei 17, 2024.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa, amekitaka Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania kufanya jitihada za kujitanua katika mafunzo hayo ya TEHAMA kwa walemavu ili kuwafikia hata waliopo katika sehemu mbalimbali za nchi ili kutanua wigo wa matumizi ya TEHAMA kwa makundi hayo ya walemavu.

Akiongea katika maonesho hayo Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Uongozi na Menejimenti katika Teknolojia ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Catherine Mkude, amemshukuru Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mh. Nape Nnauye, kwa kutoa mwaliko kwa chuo hiki kushiriki maonesho haya.

Dkt. Mkude, ameongeza kuwa maonesho haya yamekuza wigo wa ufahamu wa elimu ya TEHAMA kwa walemavu kwa viongozi na wabunge ambao watakwenda kuwafahamisha wananchi katika majimbo yao.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Mkundwe Mwasaga, amesema uwepo wa maonesho haya umekuza nafasi za mashirikiano baina ya taasisi ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Teknolojia ya Mawasiliano nchini kwa taasisi hizo kuangalia maeneo muhimu wanayoweza kushirikiana.
Maonesho ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari yanafanyika katika viwanja vya bunge jijini Dodoma, kuanzia Mei 16 na yatamalizika Mei 17, 2024 ambapo wizara hiyo hutoa nafasi kwa taasisi zinazotoa huduma za teknolojia ya habari kuonyesha huduma zao kwa viongozi na wabunge wakati bajeti ya wizara hiyo inaposomwa na kujadiliwa bungeni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news